DC Kaminyoge awaonya wafugaji, awasisitiza kufuga kisasa.

MKUU wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge akizungumza na wananchi waliojitokeza kwenye zoezi la upandaji wa miti katika shule ya sekondari Zanzui.

 


Na Samwel Mwanga,Maswa.

 

MKUU wa wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu, Aswege Kaminyoge amepiga marufuku mifugo yote kuzurura ovyo mjini Maswa badala yake wanaohusika wafuge kisasa kwa kufuga ndani au wapeleke mifugo yao nje ya mji.

 

Pia amewataka viongozi wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Maswa kuchukua hatua kwa kukamata mifugo yote ambayo inachungwa kwenye maeneo ya mji huo kwani ni kinyume cha sheria.

 

Ametoa agizo hilo wakati wa uzinduzi wa kampeni ya upandaji wa miti 1,500,000 katika wilaya uliofanyika katika shule ya sekondari Zanzui.

 

Amesema kuwa alikwisha kutoa agizo hii ni mara ya pili mara baada ya kukutana na wafugaji wenye mifugo katika mji huo pamoja na viongozi wa Ofisi ya Mamlaka hiyo wakiwemo watendaji na Wenyeviti wa vitongoji na Watendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa  kutokana na uharibifu wa mazingira unaofanywa na mifugo hiyo na tukakubaliana kufuata sheria.

 

Amesema kuwa katika kutekeleza agizo hilo tatizo liko kwa watendaji wa serikali ambao wamekuwa wakiogopa kukamata mifugo hiyo ambayo kwa sasa imekuwa ikichungwa hadi kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya na kwenye Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo.

 

“Nilikwisha kutoa maagizo kwanza nilikaa na wafugaji wa mji wa Maswa kuhusiana na uharibifu wa mazingira unaotokana na uchungaji holela wa mifugo katika mji wetu kimsingi walikubali kwamba sheria ipo na tutaitekeleza lakini tatizo liko kwetu sisi watumishi wa serikali ambao wanasimamia sheria hizi wananchi hawajakataa,”

 

“Tulikutana wote akiwemo Afisa Mtendaji wa Mamlaka ya mji wetu wa Maswa, Wenyeviti wa vitongoji wa mamlaka ya mji wetu wa Maswa, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa lakini leo hii ngombe zinachungwa hadi ofisini kwa Mkurugenzi hadi ofisi ya Mkuu wa wilaya lakini hakuna ambaye anayekubali kuchukua hatua  kwa sababu anaona kama atalaumiwa au atalalamikiwa usipochukua hatua hata kama unasali kwa kupiga magoti na  kusugua magoti hiyo ni dhambi kwa sababu tu hukuchukua sheria,”amesema.

 

Dc Kaminyoge amesema kuwa anatoa agizo jingine kwa wafugaji wote kutekeleza mambo yote ambayo walikubaliana juu ya mifugo yao kuwepo mjini huku akionya miti iliyopandwa isiguswe wala kuliwa na ng’ombe wala mbuzi.

 

“Nitoe tamko tena leo wafugaji wote mnaofuga mjini tulishakubaliana tukiwa wote na viongozi wa Mamlaka ya mji mdogo wa Maswa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa  nini cha kufanya na wafanye nini na wao walikubali sasa ni utekelezaji tu nataka kuanzia leo hii miti tuliyopanda  tuahakikishe haiguswi au hailiwi na ngombe wala mbuzi,”amesema.

 

Baadhi ya wananchi wakizungumzia maagizo hayo ya Mkuu wa wilaya waliyaunga mkono huku wakiwatupia lawama Watendaji wa mamlaka ya Mji mdogo wa Maswa kupitia  kitengo cha sheria wakidai kuwa hakifanyi kazi yake ipasavyo.

 

Wamesema kuwa iwapo kitengo hicho kingetimiza majukumu yake agizo hilo la Mkuu wa wilaya lingekuwa limetekelezwa muda mrefu lakini kwa sasa mifugo mingi inazagaa mji na hakuna hatua zozote zinazochukuliwa huku wengine wakidai mifugo hivyo ni ya baadhi ya viongozi wa kisiasa.

 

“Kitengo cha sheria kile cha Mamlaka ya Mji mdogo wa Maswa na hata cha Halmashauri ya wilaya ya Maswa vingekuwa vinawajibika hili agizo la Mkuu wa wilaya lingekuwa limetekelezwa lakini hadi sasa kiongozi naye anashangaa kutotekelezwa kwa sheria ambayo ipo na kigugumizi kipo kutokana na ng’ombe zinazochungwa hapa mjini ni za viongozi wa kisiasa hivyo wanaogopa kuwachukulia hatua,”amesema George John.

 

Wamesema kuwa japo sheria ya kuadabisha wanaoachia mifugo yao kuzurura ovyo mjini ipo lakini mamlaka za serikali zipo na hakichukui hatua yoyote kali dhidi ya wakorofi hao na ndiyo maana mifugo inachungwa hadi kwenye ofisi za serikali.

 

Katika hatua nyingine,Mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge ameagiza kupandwa miti katika bonde la mto Sola na dakio la maji la mto huo ambao umekuwa ukipeleka maji yake katika bwawa na New Sola (Maarufu bwawa la Zanzui) ambacho ndicho chanzo kikuu cha maji katika mji wa Maswa wenye wakazi wapatao 120,000 na vijiji 11 ili kuweza kutunza uhai wa bwawa hilo.

 

Amesema kuwa iwapo bado wapo wananchi wanaofanya shughuli zao karibu na dakio la maji la mto huo walipwe fidia na bonde la Ziwa Victoria ili wapishe eneo hilo kwa ajili ya uhifadhi wa bonde hilo ili kuzuia uharibifu wa mazingira ambao unaweza kusababisha madhara katika bwawa hilo kama ilivyotokea mwaka 2017 na kusababisha bwawa la New Sola kukauka.

 

“ Nalishatoa maalekezo kuwa bonde lote la mto Sola lipandwe miti  na lile dakio lote la mto Sola linalokuja na maji katika bwawa letu la Zanzui lihifadhiwe kama kuna wananchi ambao wanalima kwenye dakio na hawajalipwa fidia bonde la Ziwa Victoria lichukue hatua ya kuwafidia hao wananchi ili waondoke na waache kufanya shughuli za kilimo ili waliache kwa ajili uhai wa bwawa letu la Zanzui,”

 

“Kwa sababu  bila ya bwawa la Zanzui wananchi wa mji wa Maswa wapatao 120,000 na vijiji 11 hawatapata maji ili tuweze kuhifadhi maji kwa mwaka mzima  ni lazima tulitunze bonde hilo isiwe kama mwaka 2017 bwawa lilikauka kutokana na uharibifu wa mazingira na watu wasilime ndani ya mita 60 ya mto huo ,Maswa iko tofauti na miji mingine kwa mkoa wa Simiyu kuwa na maji ya kutosha tofauti na wilaya ya Busega na tukishindwa hivyo tutahukumiwa ni lazima tuchukue hatua,”amesema.

 

MWISHO.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa (mwenye fulana rangi ya kijani) akitoa maelezo kwa Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge(mwenye kofia)juu ya upandaji wa miti katika shule ya sekondari Zanzui.

 

Mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge (mwenye jembe) akipanda miti katika shule ya sekondari Zanzui.
 
 
 

 

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post