Jela Miaka mitatu na Fidia kwa kujeruhi Mtoto.

MAHAKAMA ya Wilaya ya Itilima.



 

Na Samwel Mwanga,Itilima.

 

MAHAKAMA ya wilaya ya Itilima katika mkoa wa Simiyu imemhukumu, Baraka Sangusangu (22) mkazi wa kijiji cha Mwamanyangu wilayani humo kwenda jela miaka mitatu na kulipa fidia ya Sh 100,000/- baada ya kupatikana na hatia ya kumjeruhi mtoto  wa kike mwenye umri wa miaka saba (jina limehifadhiwa) kwa kutumia msumali pamoja na kumchapa viboko na kumsababishia majeraha na maumivu makali sehemu mbalimbali za mwili wake.

 

Hukumu hiyo ya shauri la jinai Na.59/2023 imetolewa Novemba 6 mwaka huu na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama hiyo,Roberth Kaanwa baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashitaka.

 

Awali ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha mashitaka kutoka ofisi ya Taifa ya Mashitaka wilaya ya Itilima,Mkaguzi Msaidizi wa Polisi,Vedastus Wajanga kuwa mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo Novemba 1 mwaka huu nyumbani kwake kitongoji cha Mttambani “B” katika kijiji cha Mwamanyangu wilayani humo majira ya saa 8:30 mchana.

 

Kwa kutenda kosa la Kujeruhi ni kinyume na kifungu cha 225 cha Sheria ya Kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyo fanyiwa marejeo mwaka 2022. 

 

Mwendesha mashitaka huyo alizidi kuieleza mahakama hiyo kuwa siku ya tukio Mshitakiwa alichukua msumari ambao aliuweka ndani ya moto na kumchoma pamoja na kumchapa viboko vingi matakoni mtoto huyo ambaye ni mwanafunzi wa darasa la pili katika shule ya msingi Mwanunui iliyoko wilayani humo na kumsababishia maumivu makali sehemu mbalimbali za mwili wake.

 

Aliendelea kuieleza mahakama  hiyo kuwa baada ya mshitakiwa kufanya kitendo hicho taarifa zilifika katika kituo cha polisi na alifikishwa mahakamani na kusomewa Kosa lake na alikiri kutenda kosa hilo na vielelezo viwili vimetolewa ambavyo ni  Fomu namba tatu ya  polisi ya matibabu (PF3) na maelezo ya mshitakiwa aliyokiri mwenyewe wakati akihojiwa na kituo cha polisi.

 

Baada ya mshitakiwa kutiwa hatiani na mahakama upande wa mashtaka uliomba apewe adhabu kali ili iwe funzo kwake na kwa jamii kwani matukio kama haya huacha kumbukumbu mbaya isiyo futika kirahisi katika maisha ya mhanga na ni ukatili unaweza kuhatarisha maisha ya mhanga na hayawezi kuvumilika katika jamii .

 

Mshtakiwa alipopewa nafasi na mahakama ili aweze kujitetea aliomba mahakama impunguzie adhabu kwani ni mkosaji wa mara ya kwanza na alitenda hilo kosa hilo kwa sababu mhanga huyo ambae ni mtoto wa dada yake aliiba kiasi cha pesa Sh 2000/-.

 

Hata hivyo pamoja na utetezi huo Hakimu,Roberth Kaanwa amemhukumu mshitakiwa kwenda jela miaka mitatu na kumlipa fidia muhanga huyo kiasi cha sh 100,000/-

 

MWISHO.

 

 

 

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post