CCM yatoa Miezi miwili kukamilisha Mradi wa Maji.

Tenki la Maji lenye ujazo wa lita 50,000 linalojengwa Mtaa wa Old Maswa.


Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.

 

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Simiyu kimetoa miezi Miwili kwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kuhakikisha wanakamilisha mradi wa Maji ulioko Mtaa wa Old Maswa, Kata ya Nyakabindi, Halmashauri ya Mji wa Bariadi.

 

Aidha, Mradi huo ambao ulianza kutekelezwa tangu mwezi Januari mwaka huu, ulitakiwa kukamilika mwezi julai 2023, na kwamba hadi sasa umetekelezwa kwa asilimia 65 tu.

 

Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi wa mradi huo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa huo, Shemsa Mohammed aliwataka Wakala huo kuhakikisha wanakamilisha mradi huo kwa muda waliotaja na kufikisha maji kwa wananchi.

 

‘’Rais Samia akiwa Makamu wa Rais aliahidi kumtua mama ndoo kichwani..kufika Januari 30, 2024 nataka kuona maji yanatoka na kufika kwa wananchi ili tuwaeleeze wananchi kuwa Ilani ya CCM inatekelezwa kwa vitendo’’ alisema Shemsa.

 

Mwenyekiti huyo alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa zaidi ya shilingi Mil. 400 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa Maji ambao umelenga kunufaisha wananchi wapato 5,750 wanaoishi katika mitaa ya Old Maswa, Nyangaka na Mwahabi.

 

Alisema serikali inaendelea kuwekeza fedha nyingi katika ujenzi wa miradi ya Maji, hivyo watendaji wanatakiwa kusimamia na kukamlisha miradi hiyo kwa wakati ili wananchi waachane na kilio cha kukosa maji safi na salama.

 

Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo, Kaimu Meneja wa RUWASA wilaya ya Bariadi, Mhandisi Herry Magoti alisema mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya shilingi mil. 417.6.

 

Alisema hadi sasa kiasi cha shilingi Mil. 130.9 kimetumika, na endapo ukikamilika utatoa huduma ya maji safi na salama yatakayotosheleza wananchi wa mitaa mitatu ya Old Maswa, Nyangaka na Mwahabi.

 

‘’Mradi huu umefikia asilimia 65 na ulitarajiwa kukamilika mwezi Julai, lakini ulikwama kutokana na upatikanaji wa fedha…Mkandarasi aliondoka eneo la mradi kutokana na kucheleweshewa fedha, kwa sasa tumemlipa mkandarasi Mil. 130, na kazi ya kuleta mabomba imeanza ili tukamilishe’’ alisema.

 

Aliongeza kuwa hadi sasa ujenzi tenki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita 50,000 umekamilika, ujenzi wa vituo sita vya kuchotea maji na kioski kimoja chenye koki nne unaendelea na uchimbaji wa mitaro na ufungaji wa bomba ya kusambazi maji haujaanza.

 

Diwani wa Kata ya Nyakabindi Masanja Elias alimshukuru Dk. Samia kwa kutoa zaidi ya shilingi Mil. 417 kwa wananchi wa mitaa ya Old Mswa ili wnaanchi waondokane na adha ya maji na kwamba mrdai huo ukikamilika, Ilani ya CCM itakuwa imetekelezwa ipasavyo.

 

‘’tunajivunia kupata mradi huu wa maji, Ombi letu kwa Watendaji wa RUWASA…mradi huu ukamilike kwa wakati ili wananchi wanufaike na keki ya Dk. Samia Suluhu Hassan’’ alisema.

 

Kwa upande wao baadhi ya wananchi waliipongeza serikali kwa kutekeleza mradi wa Maji na kuiomba serikali kuharakisha ujenzi huo ili wananchi waondokane na adha ya kutafuta maji umbali mrefu.

 

Sara Nikson, Mkazi wa Nyakabindi aliishukuru serikali na kuongeza kuwa wakina mama wanahangaika kupata maji hasa nyakati za kiangazi ambapo hutumia gharama kubwa kununua ndoo za maji.

 

MWISHO. 

 

Tenki la Maji lenye ujazo wa lita 50,000 linalojengwa Mtaa wa Old Maswa.

 

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu Shemsa Mohammed, (katikati) akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi wa mradi wa Maji Old Maswa.


Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post