Wananchi watumia Ng'ombe kuvuka Mto Senani.

Watoto wakivuka Mto Senani kwa kushika mikia ya Ng'ombe.

 

Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.

 

KATIKA hali isiyokuwa na kawaida, wananchi wa Kata za Malambo, Somanda na Nyangokolwa wanalazimika kutumia ng’ombe kuvuka mto Senani kwa kuwashika mikia ili waendelee na shughuli zao kutokana na ujenzi wa daraja hilo kukwama.

 

Licha ya utekelezaji na ujenzi wa daraja hilo kuanza, lakini wananchi wanasema wanakwama kupita na kukosa huduma kutokana na mto huo kujaa maji hali inayowafanya wananchi kukosa mawasiliano.

 

‘’Wananchi wa Kata tatu za Malambo, Nyangokolwa (Matale) na Somanda wanalazimika kutumia ng’ombe kuvuka mto huu kwa kuwashika mikia ili waendelee na shughuli zao…tunaiomba serikali ikamilishe daraja hili kwa wakati’’ alisema Nyegu Nsulwa, mkazi Sanungu.

 

Akizungumza maa baada ya kukagua ujenzi wa daraja hilo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohammed aliwataka Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA) kuacha mazoea ya kuweka wakandarasi wasiokuwa na sifa ambao wanakwamisha na kuchelewesha ujenzi wa miradi ya barabara.

 

Alisema daraja hilo ni kiungo muhimu cha mawasiliano na maendeleo baina ya kata tatu za Malambo, Somanda na Nyangokolwa mjini Bariadi ambalo linajengwa kwa zaidi ya shilingi Mil. 700.

 

‘’Wakandarasi mnaowapa fedha, wanajenga chini ya kiwango, tafuteni wakandarasi wazuri…wanyimeni kazi wanaokwamisha miradi, kama fedha hakuna nitakwenda mwenyewe kuomba fedha ili daraja likamilike’’ alisema.

 

Awali akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa daraja hil, Kaimu Meneja wa TARURA Mhandisi Hussein Katakweba kwa mwaka wa fedha 2021/2022 waliidhinishiwa shilingi Mil. 420 kujenga daraja kwa awamu ya kwanza.

 

Aliongeza kuwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024 wameidhinishiwa shilingi Mil. 300 kupitia fedha za tozo ambapo mkandarasi wa awali walivunja mkataba kutokana na kuchelewesha mradi.

 

‘’Utekelezaji wa awamu ya pili kwa mwaka wa fedha 2023/24, mkataba umeanza mwezi Novemba kwa gharama ya shilingi Mil. 300 na utakamilika mwezi April 2024…ufinyu wa bajeti unafanya mradi uchelewe kukamilika’’ alisema Mhandisi Katakweba.

 

MWISHO.


 

Watoto wakivuka Mto Senani kwa kushika mikia ya Ng'ombe.
 
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu Shemsa Mohammed akiongea mara baada ya kukagua ujenzi wa daraja la Mto Senani.


Daraja la Mto Senani.

 


Nyegu Seni mkazi wa Sanungu akiongea na waandishi wa Habari (hawapo pichani) kwenye daraja la mto Senani.



Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA) wilaya ya Bariadi Mhandisi Hussein Katakweba akisoma taarifa ya ujenzi wa daraja la mto Senani, kushoto ni Meneja wa TARURA wilaya hiyo Mhandisi Mathias Mgolozi, kulia ni Ally Lufunga Afisa wa CCM Mkoa wa Simiyu.
 
 
 
 


Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post