Na Derick Milton, Itlima,
Katika kuhakikisha Mazingira ya ufundishaji na
kujifunzia yanakuwa rafiki kwa wanafunzi na walimu kwenye shule za msingi na
sekondari, Benki ya NMB imetoa samani zenye thamani ya Sh. Milioni 30 kwenye
shule tatu kwenye ya Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu.
Samani hizo ni pamoja na Meza 30, viti 30 kwa ajili ya
walimu, pamoja na madawati 130 kwa ajili ya wanafunzi kwenye shule za Msingi
Nguno, Madilana pamoja na shule ya Sekondari Ikungulipu.
Akikabidhi msaada huo, Meneja wa NMB kanda ya Magharibi
Seka Urio, amesema kuwa benki hiyo imetoa samani hizo kama kutekeleza sera yake
ya kurejesha faida kwa jamii.
Amesema kuwa NMB imekuwa ikitenga kiasi cha fedha kama
faida yake kwa ajili ya kurejesha kwa jamii, ambapo sekta ya Elimu, Afya pamoja
na majanga ndivyo vinapewa kipaumbele.
“ Tunayo furaha kubwa sana leo kama Benki kinara hapa
nchini kukabidhi samani hizi ambazo ni Meza 10, viti 10, madawati 30 kwa ajili
ya shule ya Msingi Nguno, Meza 20 na viti 20 pia kwa ajili ya shule ya
Sekondari Ikungulipu na Madawati 100 kwa ajili ya shule ya msingi Madilana,”
amesema Urio.
Ameongeza kuwa NMB itaendelea kuunga mkono juhudi za
serikali katika kuhakikisha sekta ya Elimu inaboreshwa nchini, huku akibainisha
kuwa wataendelea kutenga fedha kwa ajili ya kusaidia sekta hiyo.
Akizungumza katika Hafla ya kupokea samani hizo kwa
niaba ya Mkuu wa Wilaya ambaye alikuwa mgeni rasmi, Afisa Tawala wa Wilaya hiyo
Dinno Mwigune amewashukuru Benki ya NMB na kuhaidi kutunza samani hizo.
Mwigune ameeleza kuwa shukrani kubwa kwa NMB ni
kuhakikisha samani ambazo zimetolewa kwenye shule hizo, zinatunzwa ili ziweze
kuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi wengi.
“ Kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya niwaagize hapa walimu
wakuu wote wa hizi shule ambazo zimepokea msaada huu kutoka NMB, samani hizi
zitunzwe vyema, zidumu kwa muda mrefu ili ziweze kuwahudumia wanafunzi wengi
zaidi,” ameeleza Mwigune.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu shule ya Msingi Madilana
Niyonsaba Lameck amesema kuwa baadhi ya wanafunzi katika shule yake walikuwa
wanakaa chini hivyo msaada wa madawati 100 shuleni kwake itawezesha zaidi ya
wanafunzi 300 kukaa kwenye madawati.
“ Tunawashukuru sana NMB, msaada huu ni mkubwa sana
kwetu, zaidi ya watoto 300 kwenye shule yangu sasa wanakwenda kukaa kwenye
madawati, na tulikuwa na upungufu, sasa hautakuwepo tena” amesema Lameck.
Pendo Mabula mwanafunzi wa darasa la sita shule ya
Msingi Madilana, ameishukuru NMB kwa msaada wa madawati shuleni kwao, kwani
awali darasani walikuwa wakikaa wanafunzi wanne hadi watano kwenye dawati moja.
>>>>>>>>>>>>>Picha zaidi>>>>
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com
Post a Comment