DC Simalenga atak​a Jimbo la Bariadi kugawanywa.

 

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Simon Simalenga akiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, wakipokea Ramani yenye Matokeo ya Sensa ya watu na Makazi 2022, kutoka kwa Meneja Idara ya Mifumo ya Kijiografia wa Ofisi ya Taifa Takwimu (NBS) Benedict Mugambe.


Na Derick Milton, Bariadi.

 

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu Simon Simalenga amesema kuwa, Wilaya hiyo inalo Jimbo moja la Bariadi, ambalo ameeleza linatakiwa kugawanywa na yawe majimbo mawili ili kuweza kuletea Maendeleo ya haraka wananchi wananchi wa Wilaya hiyo.

 

Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa Jimbo hilo linavyo vigezo vyote vya kugawanywa, ambapo kigezo cha kwanza ni wingi wa watu kwani kwa mujibu wa sensa ya watu na Makazi 2022 Jimbo hilo lina jumla ya watu 644, 312.

 

Simalenga ametoa kauli hiyo Jana wakati wa mafunzo ya matokeo ya sensa ya watu na Makazi 2022, yaliyoendeshwa na Ofisi ya Taifa ya takwimu (NBS) kwa viongozi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.

 

Amesema kuwa moja ya vigezo vinavyounda Jimbo ni idadi ya watu, na kanuni zinataka Jimbo moja la uchaguzi lisiwe na watu zaidi ya Laki nne (400,000), ambapo Jimbo la Bariadi limezidi idadi hiyo.

 

Mbali na hilo Simalenga alisema kuwa katika sheria hizo, zinataka Jimbo lisiwe na Halmashauri zaidi ya Moja, ambapo Jimbo la Bariadi linalo Halmashauri mbili ambazo ni Halmashauri ya Mji na Bariadi Vijijini.

 

Alisema kuwa kwa vigezo hivyo, Jimbo la Bariadi linatakiwa kugawanywa ili kuweza kurahisisha shughuli za maendeleo kuweza kuwafikia wananchi wake kwa haraka na kwa viwango vinavyotakiwa.

 

“ Kuna baadhi ya watu na viongozi wameanza kupinga Jimbo hili kugawanywa, wanakataa kwa maslai yao wenyewe, hawajali maendeleo ya watu, kwa hali ilivyo na maendeleo ya wananchi wetu jimbo hili linatakiwa kugawanywa” alisema Simalenga...

 

“ Moja ya faida ya kuligawa jimbo Bajeti yake itakuwa kubwa, hasa fedha zinazoletwa na serikali kuu, ambapo eneo la kwanza tutakuwa na bajeti kubwa ya miundombinu ya Barabara zetu hasa za vijijini” alisema Simalenga.

 

Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wale wote wanaopinga kugawanywa kwa jimbo hilo, kutanguliza maslai mapema ya wananchi wa Wilaya hiyo pamoja na kusukumwa na utashi wa Maendeleo kwa wananchi wao.

 

Aliongeza kuwa Bado wananchi wa Wilaya hiyo wanazo changamoto nyingi hasa za mahitaji ya huduma za kijamii, ambapo ili kuweza kutatua changamoto hizo lazima maamuzi yafanyike na jimbo hilo ligawanywe.

 

Kwa upande wake Meneja Idara ya Mifumo ya Kijiografia kutoka NBS Benedict Mugambe, amewataka watendaji wa serikali na viongozi, kuhakikisha wanatumia matokeo hayo ya sensa katika kutekeleza majukumu yao vyema.

 

Aidha Mugambe amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha wanatumia matokeo hayo, kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao ya kiulinzi, huku akiwaeleza wanayo nafasi ya kufika ofisi za Takwimu na kupewa taarifa nyeti kwa ajili ya shughuli zao.


MWISHO.

 

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post