Na Derick Milton, Bariadi.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mkoani
Simiyu Simon Simalenga amesema kuwa, Wilaya hiyo inalo Jimbo moja la Bariadi,
ambalo ameeleza linatakiwa kugawanywa na yawe majimbo mawili ili kuweza kuletea
Maendeleo ya haraka wananchi wananchi wa Wilaya hiyo.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa
Jimbo hilo linavyo vigezo vyote vya kugawanywa, ambapo kigezo cha kwanza ni
wingi wa watu kwani kwa mujibu wa sensa ya watu na Makazi 2022 Jimbo hilo lina
jumla ya watu 644, 312.
Simalenga ametoa kauli hiyo Jana
wakati wa mafunzo ya matokeo ya sensa ya watu na Makazi 2022, yaliyoendeshwa na
Ofisi ya Taifa ya takwimu (NBS) kwa viongozi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.
Amesema kuwa moja ya vigezo
vinavyounda Jimbo ni idadi ya watu, na kanuni zinataka Jimbo moja la uchaguzi lisiwe
na watu zaidi ya Laki nne (400,000), ambapo Jimbo la Bariadi limezidi idadi
hiyo.
Mbali na hilo Simalenga alisema kuwa
katika sheria hizo, zinataka Jimbo lisiwe na Halmashauri zaidi ya Moja, ambapo
Jimbo la Bariadi linalo Halmashauri mbili ambazo ni Halmashauri ya Mji na Bariadi
Vijijini.
Alisema kuwa kwa vigezo hivyo, Jimbo
la Bariadi linatakiwa kugawanywa ili kuweza kurahisisha shughuli za maendeleo
kuweza kuwafikia wananchi wake kwa haraka na kwa viwango vinavyotakiwa.
“ Kuna baadhi ya watu na viongozi
wameanza kupinga Jimbo hili kugawanywa, wanakataa kwa maslai yao wenyewe,
hawajali maendeleo ya watu, kwa hali ilivyo na maendeleo ya wananchi wetu jimbo
hili linatakiwa kugawanywa” alisema Simalenga...
“ Moja ya faida ya kuligawa jimbo
Bajeti yake itakuwa kubwa, hasa fedha zinazoletwa na serikali kuu, ambapo eneo
la kwanza tutakuwa na bajeti kubwa ya miundombinu ya Barabara zetu hasa za vijijini”
alisema Simalenga.
Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wale
wote wanaopinga kugawanywa kwa jimbo hilo, kutanguliza maslai mapema ya
wananchi wa Wilaya hiyo pamoja na kusukumwa na utashi wa Maendeleo kwa wananchi
wao.
Aliongeza kuwa Bado wananchi wa Wilaya
hiyo wanazo changamoto nyingi hasa za mahitaji ya huduma za kijamii, ambapo ili
kuweza kutatua changamoto hizo lazima maamuzi yafanyike na jimbo hilo
ligawanywe.
Kwa upande wake Meneja Idara ya Mifumo ya
Kijiografia kutoka NBS Benedict Mugambe, amewataka watendaji wa serikali
na viongozi, kuhakikisha wanatumia matokeo hayo ya sensa katika kutekeleza
majukumu yao vyema.
Aidha Mugambe amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama
kuhakikisha wanatumia matokeo hayo, kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao ya
kiulinzi, huku akiwaeleza wanayo nafasi ya kufika ofisi za Takwimu na kupewa
taarifa nyeti kwa ajili ya shughuli zao.
MWISHO.
إرسال تعليق