TFF yakabidhi mipira shule za msingi 34 Simiyu.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dkt. Yahaya Nawanda akigawa mpira kwa mwanafunzi wa shule ya Msingi Bariadi, wakati wa zoezi la kugawa mipira 1,000 iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia programu ya michezo shuleni inayotekelezwa na shirikisho la mpira Miguu Duniani (FIFA).
 



Na Derick Milton, Smiyu.

Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) limekabidhi mipira 1,000 kwa shule za msingi 34 katika mkoa wa simiyu kwa lengo la kutekeleza programu michezo shuleni iliyoanzishwa na shirikisho la mpira wa miguu Duniani (FIFA).

Akizungumza katika hafla ya kukabidi mipira hiyo kwa niaba ya Rais wa TFF, Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa miguu mkoa wa Simiyu (SIFA) Osuri Kosuri amesema kuwa mkoa huo umekuwa mnufaka wa mipira hiyo kati ya mikoa 14 Tanzania Bara na Zanzibar.

Kosuri ameeleza kuwa jumla ya shule 34 kwa mkoa wa Simiyu zitapatiwa mipira hiyo, ambapo kila shule imepangiwa kupata mipira 25 ambayo wanafunzi wataitumia wakati wa michezo.

“ Ni matumaini ya Rais wetu wa TFF kuwa mipira hii inakwenda kufanya kazi iliyokusudiwa, tunataka kuona vipaji vinaibuliwa kupitia mipira hii, TFF na FIFA watakuwa wanakuja kufanya ukaguzi kuona kama mipira hii inaleta tija,” alisema Kosuri.

Mwenyekiti huyo wa SIFA alimshukuru Rais wa TFF Wallace Karia kwa kuchagua mkoa wa Simiyu kuwa miongoni mwa mikoa ya kupata mipira hiyo, ambao alieleza chama chake kitahakikisha vipaji vinaibuliwa kupitia vifaa hivyo.

Kabla ya kugawa mipira hiyo kwa shule nufaika, Mkuu wa Mkoa huo Dkt, Yahya Nawanda alishukuru TFF, ambapo ameagiza kila shule ambayo imepokea mipira kuhakikisha inatumika kwa watu sahihi.

“ Sitegemei kuona au kusikia mipira hii inatumiwa na watu wazima, hii mipira imetolewa kwa wanafunzi wa shule za msingi, darasa la kwanza hadi la saba, tunataka kuona mkoa wa Simiyu tunatoa akina Samata wengi,” alisema Dkt. Nawanda.

Janeth Kato Mwalimu wa Michezo shule ya Msingi Bariadi, amesema kuwa katika shule hiyo walikuwa wanatumia mipira miwili, hali ambayo haikukidhi mahitaji ya wanafunzi wote shuleni hapo.

“ Tunawashukuru sana TFF kwa msaada huu, kama mwalimu wa michezo nilipata wakati mgumu kuwafundisha watoto kwa mipira miwili, leo nimepewa mipira 25, nina uhakika tutaibua vipaji vingi,” alisema Kato.

Naye Mwenyekiti wa soka la vijana mkoa Kajanja Mgengele, amesema mipira hiyo imekuja katika wakati mwafaka, kwani FIFA na TFF wamedhamilia kuibua vipaji kuanzia ngazi za chini.

“ Kama Mwenyekiti wa eneo hili, tuna uhakika kupitia mipira hii, tutakwenda kuibu vipaji halisi, ukosefu wa mipira ilikuwa changamoto kubwa, tunashukuru TFF na FIFA kwa kutatua changamoto hii, Amesema Kajanja.

MWISHO.

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post