- Kumvaa Ndaki.
Na Samwel Mwanga, Maswa.
KATIBU wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Mkoa wa Mwanza, Mwalimu Godlisten Kabarata, amejiunga rasmi kwenye mbio za ubunge kwa kuchukua fomu ya kuwania kuteuliwa kuwa mgombea wa ubunge wa Jimbo la Maswa Magharibi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Amekabidhiwa fomu hiyo jumapili Juni 29,2025 katika ofisi za CCM wilaya ya Maswa na Katibu wa CCM wilayani humo,Mwl Efreim Kolimba.
Hatua hiyo inamweka katika nafasi ya kumkabili mbunge wa sasa wa jimbo hilo, Mashimba Ndaki, ambaye pia anatarajiwa kutetea nafasi yake katika uchaguzi wa mwaka huu.
Mwalimu Kabarata ni mzoefu katika harakati za kisiasa na za kijamii akiwa ameongoza nyadhifa mbalimbali ndani ya CWT na CCM. Amewahi kuwa Mkuu wa shule Mwenyekiti wa CWT Wilaya,Katibu wa CWT Wilaya na Katibu wa CWT Mkoa wa Mwanza.
Pia amewahi kuwa Katibu wa Uchumi, Mipango na Fedha wa CCM na
Mjumbe wa Mkutano wa CCM Mkoa wa Simiyu.
Mbali na nafasi hizo, Mwalimu Kabarata pia aliwahi kuwa Mratibu wa Magufuli Club 2025 kwa majimbo ya Maswa Magharibi na Mashariki, na Katibu wa Shirikisho la Walimu Makada Mkoa wa Simiyu.
Aidha, aliwahi kugombea nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) mwaka 2017 na pia aliwania ubunge wa jimbo hilo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Akizungumza baada ya kuchukua fomu, Mwalimu Kabarata amesema anaamini uzoefu na ufuatiliaji wake katika masuala ya maendeleo ya jamii na elimu utakuwa chachu ya mabadiliko chanya kwa wananchi wa Maswa Magharibi endapo atapewa ridhaa ya kuwaongoza.
"Ni wakati wa Maswa Magharibi kupata mbunge mwenye dira mpya, anayegusa maisha ya wananchi wa kawaida kwa vitendo, si kwa ahadi tu," amesema.
Mwisho..
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com
Post a Comment