Waandishi wa Habari Simiyu watangaza kutofanya kazi na DC Bariadi.

 


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.

Tamko,

Klabu ya waandishi wa Habari Mkoa wa Simiyu (SMPC) imesikitishwa na kuuzunishwa na kitendo cha Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mkoani humo, Simon Simalenga cha kuwafukuza kwa dhihaka kwenye kikao cha Ushauri cha Wilaya (District Consultative Council -DCC), waandishi wa habari saba wa vyombo mbalimbali vya habari waliokwenda kuchukuwa taarifa kwenye kikao hicho, kilichofanyika Februari 19,2024, katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.


Waandishi hao wa habari ambao wamefikisha taarifa rasmi kwa uongozi wa Klabu ya waandishi wa habari simiyu (Simiyu Press Club) kulalamikia kitendo hicho, wamesema kitendo alichofanya mkuu huyo wa wilaya si tu kimewafedhehesha waandishi wa habari pamoja na tasnia ya habari, bali kinakiuka Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayohimiza uhuru wa mtu kutoa na kupata taarifa.

 

Halikadhalika, kitendo hicho kilichofanywa na Mkuu Wilaya Bw. Simalenga kuwafukuza waandishi wa habari tena kwa lugha isiyokuwa na staha, kinakinzana na sheria ya haki ya kupata taarifa ya mwaka 2016.

 

DC Simalenga alinukuliwa akisema: “MMEKUJA KUFANYA NINI HAPA, NILIWAAMBIA MSIALIKE WAANDISHI WA HABARI, NANI ALIALIKA TENA? WAANDISHI WA HABARI TOKENI NJE NA MILANGO YA UKUMBI IFUNGWE," mwisho wa kunukuhu.

 

Rekodi zinaonesha kuwa, hii siyo mara ya kwanza kwa kiongozi huyo kufanya vitendo hivyo, ambapo mara ya kwanza aliwatolea maneno ya kudhalilisha viongozi wa SMPC, ambao ni Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wetu.

 

Kutokana na hali hiyo, Klabu ya waandishi wa Habari Mkoa wa Simiyu (SMPC) kwanza inatangaza kulaani kitendo cha udhalilishaji kilichofanywa na DC Simalenga kwa waandishi wa habari Mkoa wa Simiyu.

 

Pili, Uongozi wa SMPC na waandishi wake inatangaza rasmi kuanzia leo 20 Februari,2024,hautafanyakazi na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Simon Peter Simalenga.

 

Tatu, tunaiomba Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kutoa tamko juu ya tukio hilo.

 

Hivyo basi, tunawaomba viongozi mbalimbali na wananchi ndani ya Mkoa wa Simiyu, kuwaheshimu waandishi wa habari pale wanapotekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria, na kuepuka kuwafanyia vitendo vya unyanyasaji, ubaguzi, udhalilishaji na ukikwaji wa sheria.

 

Imetolewa na Uongozi wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Simiyu (SMPC).

 

20 FEBRUARI,2024.

 


Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post