TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI.
Tamko,
Klabu ya waandishi wa Habari Mkoa wa Simiyu (SMPC)
imesikitishwa na kuuzunishwa na kitendo cha Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mkoani
humo, Simon Simalenga cha kuwafukuza kwa dhihaka kwenye kikao cha Ushauri cha
Wilaya (District Consultative Council -DCC), waandishi wa habari saba wa vyombo
mbalimbali vya habari waliokwenda kuchukuwa taarifa kwenye kikao hicho,
kilichofanyika Februari 19,2024, katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Waandishi
hao wa habari ambao wamefikisha taarifa rasmi kwa uongozi wa Klabu ya waandishi
wa habari simiyu (Simiyu Press Club) kulalamikia kitendo hicho, wamesema kitendo alichofanya mkuu huyo wa wilaya si tu kimewafedhehesha waandishi
wa habari pamoja na tasnia ya habari, bali kinakiuka Ibara ya 18 ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayohimiza uhuru wa mtu kutoa na kupata taarifa.
Halikadhalika, kitendo hicho
kilichofanywa na Mkuu Wilaya Bw. Simalenga kuwafukuza waandishi wa habari tena
kwa lugha isiyokuwa na staha, kinakinzana na sheria ya haki ya kupata taarifa
ya mwaka 2016.
DC
Simalenga alinukuliwa akisema: “MMEKUJA
KUFANYA NINI HAPA, NILIWAAMBIA MSIALIKE WAANDISHI WA HABARI, NANI ALIALIKA
TENA? WAANDISHI WA HABARI TOKENI NJE NA MILANGO YA UKUMBI IFUNGWE," mwisho
wa kunukuhu.
Rekodi zinaonesha kuwa, hii siyo mara
ya kwanza kwa kiongozi huyo kufanya vitendo hivyo, ambapo mara ya kwanza
aliwatolea maneno ya kudhalilisha viongozi wa SMPC, ambao ni Mwenyekiti na
Makamu Mwenyekiti wetu.
Kutokana na hali hiyo, Klabu ya
waandishi wa Habari Mkoa wa Simiyu (SMPC) kwanza inatangaza kulaani kitendo cha
udhalilishaji kilichofanywa na DC Simalenga kwa waandishi wa habari Mkoa wa
Simiyu.
Pili, Uongozi wa SMPC na waandishi
wake inatangaza rasmi kuanzia leo 20 Februari,2024,hautafanyakazi na Mkuu wa
Wilaya ya Bariadi, Simon Peter Simalenga.
Tatu, tunaiomba Wizara ya Habari, Mawasiliano
na Teknolojia ya Habari kutoa tamko juu ya tukio hilo.
Hivyo basi, tunawaomba viongozi
mbalimbali na wananchi ndani ya Mkoa wa Simiyu, kuwaheshimu waandishi wa habari
pale wanapotekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria, na kuepuka kuwafanyia
vitendo vya unyanyasaji, ubaguzi, udhalilishaji na ukikwaji wa sheria.
Imetolewa na Uongozi wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Simiyu
(SMPC).
20 FEBRUARI,2024.
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com
إرسال تعليق