Na COSTANTINE MATHIAS, Maswa.
SERIKALI kupitia Wizara ya kilimo imesambaza Boom Spray (Maboza) na ndege zisizokuwa na Rubani (Drones) kwa ajili ya kunyunyuzia mashamba ya wakulimwa wa Pamba ili kudhibiti wadudu wanaoshambulia zao hilo.
Zana hizo za kisasa zimetolewa na serikali kwa wakulima kupitia Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) inayotekelezwa na serikali ili kuongeza tija kwenye kilimo na kwamba zana hizo zitahudumia wakulia bure.
Akizungumza juzi wakati wa kukabidhi zana hizo, Afisa Kilimo wilaya ya Maswa, kutoka Bodi ya Pamba nchini (TCB) Mabrouk Ally amesema wameanzisha Programu Maalumu katika vijiji vya kata ya Senani wilayani Maswa Mkoani Simiyu ambayo inatekeleza mradi wa Jenga Kesho iliyo Bora na kwamba mradi huo umeongeza nguvu kwa kuajiri maafisa kilimo.
‘’Mradi huu umeleta maafisa kilimo katika kata hii kwa kila kijiji ili kuwafikishia huduma wakulima na kuwaelekeza kanuni za kilimo…Mradi huu pia umekuja na vifaa kwa ajili ya kilimo ikiwemo Matrekta kwa ajili ya kulimia, zana za kupulizia (boom spray), ndege zisizo kuwa na rubani (drones) na mabomba ya mgongoni ambayo yatakuwa kwenye kata hii ili wakulima waazime kwenda kutumia na kurudisha’’ anasema Mabrouk.
Anasema, Lengo la Mradi huo ni kuifanya Kata ya Senani na vijiji vingine vyenye mradi huo kutumika kama sehemu ya vyanzo vya zana za kilimo ikiwemo Trekta, Ndege zisizo na rubani, Jembe la Kupandia na kupalilia watavipata katika eneo moja kwa kuazima na kurejesha baada ya kutumia bila malipo yoyote.
Anafafanua kuwa huduma ya ndege zisizo na rubani, mjaembe ya kulimi na kupandia pamoja na maboza ya kupulizia pamba yanatolewa bure ambapo wananchi wanatakiwa kufuata utaratibu wa serikali kupitia watendaji wa vijiji ili kila pamba inayopandwa inavunwa.
‘’Kila Kijiji kitakuwa na kila aina ya kifaa (zana) za kilimo na kila mkulima atanufaika…ukiamka unataka kwenda kupulizia shamba kwa kutumia bomba la mgongoni litakuwepo ofisi ya Mtendaji, ukihitaji kupulizia kwa drone itakuwepo na mtaalamu nitakuwepo, ukiwa na shamba kubwa ukahitaji Boza litakuwepo na utaambatana na mtaalamu’’ anasema.
Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kutoka Halmshauri ya Wilaya ya Maswa, Robert Urasa anasema wanamshukuru Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa vifaa vya kisasa kwa ajili ya kudhibiti visumbufu vya zao la pamba.
Anasema changamoto kubwa ya kudhibiti wadudu ilikuwa inawapata wakulima wengi, licha ya serikali kutoa madawa lakini wakulima walikuwa wanashindwa namna sahihi ya kudhibiti wadudu hao.
‘’Wakulima walikuwa wanahangaika kubeba mabomba mgongoni hususani wenye mashamba makubwa wakuliwa wanashindwa kudhibiti wadudu, lakini vifaa hivi vitawarahisishia wakulima namna ya kupulizia wadudu shambani na kudhibiti wadudu kwa wakati’’ anasema Urasa.
Mkulima Mwezeshaji anayehudumia kata 17 za Tarafa ya Mwagala, Lupande Nilla anawataka wakulima kujiandaa kuzalisha pamba baada ya serikali kutatua changamoto ya kudhibiti wadudu wanaoharibu zao la Pamba.
Anasema wakulima wenye mashamba makubwa walikuwa wanashindwa kudhibiti wadudu wakati wa upuliziaji kutokana na kuchoka kubeba matabi mgongoni lakini baada ya serikali kuwarahisishia watatunza vifaa hivyo na watazalisha kwa tija.
Elizabeth Mahangila kutoka kijiji cha Bushashi anampongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kugawa zana za kilimo za kisasa ambazo zitawasaidia kuongeza uzalishaji na pia watakabiliana na wadudu kwa wakati.
Mkuu wa Wilaya ya Maswa Aswege Kaminyoge anasema ameridhishwa na matumizi ya zana za kilimo kwa ajili ya upuliziaji wa wadudu kwenye zao la pamba huku akiipingeza serikali ya awamu ya sita kwa kutekeleza ahadi hiyo.
‘’Kwa niaba ya Wananchi wa wilaya ya Maswa, tunatoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan pamoja na Waziri wa Kilimo (Bashe) na wasaidizi wake, wananchi wa Wilaya ya Maswa wamefarijika na Utendaji wa serikali ya awamu ya sita chini ya Utekelzaji wa Ilani ya CCM’’ anasema na kuongeza.
‘’Hakika Utekelezaji wa Ilani ya CCM unaonekana kwa vitendo kwa serikali, sijawahi kuona miujiza ya namna hii kwa kupulizia dawa kwa kutumia drones zikiwa na dawa na zinapuliza mvuke unaoenda kuingia moja kwa moja kwenye majani na hakuna mdudu atakayebaki anashambulia pamba’’.
Anawataka viongozi watakaohusika na ugawaji wa vifaa vya kilimo kwa wakulima, wasifanye urasimu na badala yake watende haki kwa wakulima ili kila mmoja anufaika na matunda ya serikali ya Dk. Samia Suluhu Hassan.
‘’Wasione wakulima wengine hawafai kwa namna yoyote ile, awe maskini, awe tajiri, kijana, mama au baba…wote wapate fursa sawa kutumia vifaa hivi ambapo Rais Dk. Samia ametoa bila kujali hali zao kiuchumi au mwana chama wa Amcos, wote wapate haki sawa na kwa wakati’’ anasisitiza Kaminyoge.
MWISHO.
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com
Post a Comment