Barabara ya Mzunguko (Roud About) iliyojengwa na Wakala wa Barabara (TANROADS) katika Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu.
Na COSTANTINE MATHIAS, Simiyu.
Serikali kupitia Wakala ya Barabara (TANROADS) Mkoa wa Simiyu imeendelea
kutekeleza miradi mikubwa mitano ya ujenzi wa Barabara na Madaraja ili kufungua
fursa za Uchumi, Usafiri na Usafirishaji.
Akizungumza na Waandishi wa Habari juzi, Meneja wa Wakala huo, Mhandisi
Boniface Mkumbo amesema mafanikio hayo ni Utekelezaji wa Ilani ya CCM chini ya Serikali
ya awamu ya sita katika sekta ya ujenzi.
Amesema, Serikali kupitia TANROADS imefanikiwa kukamilisha ujenzi wa awamu ya
tatu ya kipande cha barabara ya Bariadi-Maswa yenye urefu wa Kilometa 49.7
pamoja na Barabara ya mchepuo ya Maswa (Maswa Bypass), Lamadi-Bariadi-Maswa-Wigelekelo
hadi Mwigumbi upande wa Shinyanga na Daraja la Malampaka lenye mita 12.5.
Amefafanua kuwa miradi mingine ambayo ipo kwenye hatua za upembuzi yakinifu kwa
ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami ni Barabara ya Bariadi-Salama-Ngh’aya-Magu
(Km 76) inayounganisha mkoa wa Simiyu na Mwanza, Barabara ya Nyashimo-Ngasamo-Dutwa
(km 48), na mradi mkubwa wa ujenzi wa Barabara ya Karatu-Mbutu-Hydom-Mto
Sibiti-Meatu-Lalago-Maswa yenye Jumla ya kilometa 339.
‘’Madaraja zaidi ya 20 yamejengwa katika mtandao wa barabara kwa
gharama ya Shilingi Bil. 5.6 na Ujenzi wa Daraja kubwa kwenye mto Itembe
lenye urefu wa mita 150 unaendelea, ujenzi wake umefikia asilimia 75…daraja
hilo linaunganisha Mkoa wa Singida, Mikoa mingine ya Kanda ya kati na kanda ya
kaskazini’’ amesema Mhandisi Mkumbo.
Ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa
na Dk. Samia Suluhu Hassan zaidi ya taa 569 za barabarani zimefungwa kwenye
miji na Vijiji vikubwa ili kuwafanya wananchi kuendelea na shughuli zao za
kiuchumi na kijamii hata giza linapoingia.
Aidha, Mhandisi Mkumbo ameishukuru Serikali kwa kuweza kuwajali Wakandarasi
Wazawa ambapo Mkoa wa Simiyu ni Moja kati ya Mikoa ambayo kazi nyingi wamepewa
Wakandarasi wa ndani na kuwapa Kipaumbele Wanawake ili kuweza kuwawezasha
kupewa upendeleo ili kuwakuza kiuchumi.
Mhandisi Mkumbo amewataka Wananchi kutunza Miundombinu ya Barabara kwani Serikali inatumia fedha kuhakikisha wananchi wanapita kwenye Miumbombinu iliyo na viwango vinavyokubalika.
Kwa upande wake Mwakilishi wa kampuni ya Rocktronic Ltd inayotekeleza ujenzi wa daraja la Mto Itembe, Mhandisi David Sanagala anamshukuru Rais Samia na serikali yake kwa kuendelea kuwaamini wakandarasi wazawa ambao wanatekeleza miradi ya ndani kwa kuzingatia viwango, ubora na wakati.
Amesema kukamilika kwa daraja la Mto Itembe lenye urefu wa mita 150 linalounganisha wilaya za Meatu (Simiyu) na Mkalama (Singida) litafungua fursa za uchumi na pia litarahisisha mawasiliano.
Anawataka wakandarasi wazawa kujiamini na kuzingatia viwango, Ubora na kutekeleza mradi kwa wakati ili serikali iweze kuendelea kuwaamini.
Jibunge Mtaba Mkazi wa kijiji cha Bukundi wilayani Meatu anaishukuru Serikali kwa kujenga daraja hilo ambalo limekuwa mkombozi kwa wananchi, wasafiri, mifugo na wakulima kusafirisha mazao yao.
‘’Tulikuwa tunasombwa na maji hapa, mto ukijaa tulikuwa tunashindwa kupita, tunaishukuru serikali kwa kujenga daraja la Mto Itembe ambalo litarahisisha mawasiliano, usafiri na usafirishaji wa bidhaa na mazao…tunaishukuru serikali ya Dkt. Samia kwa kutoa fedha’’ anasema Jibunge.
MWISHO.
Ujenzi wa Barabara ya Mzunguko (Roud About) katika Mji
wa Lamadi wilayani Busega Mkoani Simiyu unaotekelezwa na Wakala wa
Barabara (TANROADS) ukiendelea.

Post a Comment