Na Derick Milton, Simiyu.
Ungozi wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Simiyu
(SMPC) Kupitia kwa mwenyekiti wake Frank Kasamwa umetangaza rasmi leo, kumalizika
kwa tofauti zilizokuwepo kati ya waandishi wa Habari wa Mkoa huo na Mkuu wa
Wilaya ya Bariadi Simon Simalenga.
Katika taarifa iliyotolewa leo na uongozi wa Klabu hiyo
ikisaniwa na Mwenyekiti Kasamwa, ilieleza kuwa hatua hiyo imekuja baada ya
kikao cha maridhiano ambacho kilifanyika jana Machi 10, 2024 mjini Bariadi.
Ilielezwa kuwa kikao hicho kiliitishwa na Umoja wa
Klabu za waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) Chini ya Rais wake Deogratius
Nsokolo, ambapo kiliwakutanisha waandishi wa Habari na Mkuu wa Wilaya hiyo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa kikao hicho kilihudhuriwa
pia na Mkurugenzi Msaidizi Habari Maelezo Bi Zamaradi Kawawa, Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu Dkt. Yahaya Nawanda pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC Keneth
Simbaya.
“ Uongozi wa SMPC unatangaza kuwa kufuatia kikao hicho
tumekubaliana kuondoa tofauti zilizokuwepo baina yetu na Mkuu wa Wilaya,
tumekubaliana kushirikiana na kwamba kila upande utafanya kazi kwa kuzingatia
mipaka ya kazi yake bila ya kuathiri upande mwingine kwa manufaa ya umma,”
ilisema taarifa hiyo.
Ikumbukwe Februari 20, 2024 Klabu hiyo ilitoa tamko la
kulaani tukio lililodaiwa kufanywa na Mkuu huyo wa Wilaya la kuwafukuza
waandishi wa habari watano katika kikao cha ushauri cha Wilaya (DCC)
kilichofanyika Februari 19, 2024.
Katika tamko hilo, Klabu hiyo ilitangaza kuwa waandishi
wa Habari wa Mkoa huo ambao ni wanachama wake, hawataandika tena Habari za Mkuu
huyo wa Wilaya kutokana na kitendo chake kuwadharirisha wandishi wa Habari.
Klabu hiyo imeishukuru Wizara ya Habari na Teknologia
ya Habari, Uongozi wa Mkoa wa Simiyu pamoja na Viongozi wa Umoja wa Klabu za
waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) kwa kuingilia kati suala hilo na kuweza
kulipatia ufumbuzi.
MWISHO.
Post a Comment