Na COSTANTINE MATHIAS,
aliyekuwa Tanganyika.
BAADA ya Serikali kupitia Bodi ya Pamba nchini (TCB) kutangaza bei elekezi ya kununua zao hilo kuwa ni shilingi 1,150 katika msimu wa 2024/25, wakulima wa pamba wametakiwa kuzingatia uvunaji Bora na kuhifadhi ili kulinda ubora wa zao hilo.
Aidha wametakiwa kututumia mifuko ya sandarusi kuvuna na badala yake watumie mifuko inayotolewa na Bodi ya Pamba ili kuendelea kulinda ubora wa zao hilo.
Hayo yalibainishwa hivi karibuni na Bibi Shamba wa Kampuni ya NGS Mkoani Katavi wakati akikagua mashamba ya wakulima ambapo aliwataka kutoharibu pamba kwa kuchanganya na maji, mchanga na mafuta ili kuongeza uzito.
Alisema wanawatembelea na kuwashauri wakulima hatua mbalimbali za kilimo Cha pamba ikiwemo kupanda, kupalilia, kupulizia, kuvuna hadi kuhifadhi na kuendelea kulinda ubora.
"Tunawashauri wakulima wetu wakati wa uvunaji wasitumie mifuko ya sandarusi, Kuna mifuko maalumu inayotolewa na Bodi ya Pamba na tunaisambaza kwa wakulima ili iwasaidie wakati wa uvunaji" alisema Asegelile.
Aliwataka pia kutochafua pamba kwa kuchanganya maji, mchanga, mafuta na manyoya ili kuongeza uzito wapate fedha nyingi jambo ambalo linaharibu ubora wa pamba.
Mkaguzi wa Bodi ya Pamba Mkoa wa Katavi Philibert Bugelaha alisema wamejipanga kusimamia ununuzi ili mkulima apate haki yake ikiwemo kuangalia Hali na usimamizi wa vituo vya kukusanyia pamba.
Aliwahakikisha wakulima na wanunuzi kuwa watasimamia ili kila mmoja aweze kupata haki yake ikiwemo kusimamia Hali ya vituo na manunuzi ili kila mmoja apate anachostahili.
Aliongeza kuwa wamejipanga kusimamia ubora wa zao hilo la kimkakati ili kuendelea kulinda ubora kwa sababu pamba inategemewa kwenye soko la kimataifa.
Amewasisitiza wakulima kusimamia ubora na usafi wa pamba ili kulinda ubora wa zao hilo la kimkakati na kwamba soko la uhakika lipo na watapatiwa fedha baada ya mauzo.
Wakulima wa pamba Mkoani humo waliipongeza serikali kwa kuwasogezea huduma za ugani huku wakiahidi kuongeza tija na uzalishaji.
"Tunashukuru serikali kwa kuendelea kutupatia pembejeo ya zao la pamba, nasi tunaahidi kuongeza tija na uzalishaji" alisema Robart Kazungu mkazi wa Kapanga.
MWISHO.


Post a Comment