Na COSTANTINE MATHIAS, Busega.
June 13, kila mwaka huadhimishwa siku Maalumu kwa ajili ya kujenga uelewa juu ya Masuala yanayohusu Watu wenye Ualbino ambpo katika Mkoa wa Simiyu yamefanika katika kituo cha Bikra Maria Msaada wa Damia kilichopo Lamadi wilayani Busega.
Kituo hicho ambacho hulea watoto wenye mahitaji maalumu ikiwemo wenye Ualbino, mtindio wa Ubongo, Ulemavu wa viungo pamoja na watoto wanaotupwa.
Akizunguma kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi wa kituo hicho Sista Helena Maria amesema Watu wenye Ualbino wanatakiwa kulindwa na pia wanayo haki ya kuishi kama watu wengine.
Ameeleza kuwa, ni aibu kumwondolea uhai binadamu au kuona mtoto mdogo akiachishwa masikio, kichwa na mikono wakati huo akiipongeza serikali ya mkoa wa Simiyu pamoja na viongozi wote kwa kudhibiti hali hiyo.
‘’Juzijuzi matukio mawili ya ukatili yametokea Geita na Kagera tumesikia, lakini tunaendelea kuomba Tanzania yetu popote pale walipo wenye Ualbino na walemavu wengine…ulinzi uimarishwe, tusikomee jeshi la Polisi tu na wazazi tuwe walinzi kwa watoto wetu’’ amesema Sista Helena.
Amewaomba Watanzania wenye mapenzi mema kuendelea kupinga ukatili huo lakini pia kuweka Ulinzi ili watu wenye Ualbino waweze kuishi kama watu wengine kwa sababu wana uwezo na haki kama binadamu wengine.
Katibu Tawala, Wilaya ya Busega Sangayi Mambai, aliyemwakilisha Mkuu wa wilaya hiyo, amesema kuwa serikali ya Dk. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuwa walinda watu wenye Ualbino pamoja na makundi maalumu kwa nguvu zote.
Ameitaka jamii kuondokana na Imani potofu huku serikali ikindelea kuzikema pamoja na kutoa elimu kwa wananchi ili watambue kuwa Watu wenye Ualbino wana haki na Uhuru wa kuishi kama binadamu wengine.
‘’Tuendelee kuwa mabalozi wa kuwalinda na kuwasemea popote pale tunapopata nafasi…Nitoe rai kwa wananchi wa Mkoa wa Simiyu, viongozi wa vijiji, kata na wilaya, tusimamie na kuwasidia wenye ualbino kwa sababu wana haki kama watu wengine, Amani na Uhuru wao ni kama wa Mtanzania mwingine’’ amesema Mambai.
Mratibu wa kituo hicho, Belensi China amesema kituo hicho kilianzishwa mwaka 2011 hadi sasa kuwa watoto 83 wakiwemo wenye Ualbino, mtindio wa Ubongo, walemavu wa viungo pamoja na watoto waliotupwa jalalani.
Katibu Mkuu wa Albinism Sports Club Joseph Sinda, amesema wanaipongeza serikali kwa kutenga siku maalumu kwa ajili ya kuongeza uelewa kwa Watu wenye Ualbino kwa sababu wenye Ualbino ni sawa na watu wengine wasio na Ualbino.
Ameitaka serikali kuwapa haki sawa ikiwemo kuwashirikisha katika shughuli za kiuchumi, kijamii na kisiasa pamoja na kuwapa fursa sawa katika ajira huku akiiomba serikali kudhibiti wimbi la mauaji na ukatili unaoendelea dhidi ya Watu wenye Ualbino.
‘’Tunamwomba Rais Samia atoe tamko, hili wimbi linataka kujirudia tena ili kuichafua nchi yetu…atoe tamko ili mtu yeyote atakayekutwa, kukamatwa au kuthibitika achukuliwe hatua kali ikibidi sheria ya kunyongwa itekelezwe sababu naye ameondoa uhai wa mwenzake’’ amesema Sinda.
Amewaomba viongozi wa Mikoa na Wilaya kuimarisha ulinzi dhidi ya watu wenye ualbino huku akiwataka wazazi na walezi kusimamia malezi pamoja na kuwapenda watoto wao.
Mkaguzi wa Polisi wilaya ya Busega Musa Mondo ambaye pia ni Polisi Jamii wa Wilaya hiyo, amewahakikishia kuwa wataimarisha ulinzi na malezi katika kituo hicho huku akiwataka wazazi na walezi kutoa taarifa wanaposikia vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidhi ya watu wenye Ualbino na wengineo.
MWISHO.
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com
Post a Comment