Serikali yabaini Ekari hewa elfu 40 za Pamba Bariadi.

Zao la Pamba.


 

Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.

 

SERIKALI kupitia Bodi ya Pamba nchini (TCB) imegawa dawa kwa ajili ya kupulizia zao la pamba kwa ekari hewa elfu 40 ili kudhibiti wadudu wanaoshambulia zao hilo wilayani Bariadi Mkoani Simiyu.

 

Aidha imeelezwa kuwa kuna baadhi ya wakulima wasiokuwa waaminifu ambao walikuwa wanachukua dawa hizo, kwa ajili ya kuzitumia katika kilimo cha bustani au kuziuza ili waweze kupata fedha.

 

Hayo yamebainishwa leo na Mkuu wa wilaya hiyo Simon Simalenga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mazao wilayani humo, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Mwamlapa kata ya Kasoli, ambapo amesema katika msimu ujao hakuna mkulima atakayechukua dawa bila kuonyesha shamba lake.

 

Simalenga amefafanua kuwa katika zoezi hilo kila mkulima atapigwa picha ikiwemo kuonyesha shamba lake ili kuondoa hasara kwa serikali juu ya ununuzi wa dawa ambazo zinapelekwa na wakulima katika matumizi mengine.

 

‘’aliyelima ekari nyingi anakosa dawa, na ambaye hakulima anapata dawa na kuziuza, tunawanyima haki wanaojitoa kulima pamba kwa sababu wanaochukua dawa si waliolima…Kwa wilaya ya Bariadi, msimu uliopita zaidi ya ekari hewa elfu 40 zimepatikana kwa wananchi kuchukua dawa wakati hawajalima pamba’’ amesema Simalenga na kuongeza.

 

‘’kwa msimu ujao, hakuna mkulima atakayechukua dawa bila kuonyesha shamba lake na atapigwa picha ili dawa wapewe waliolima pamba pekee na siyo kila mtu…bei elekezi ya pamba imetolewa hakuna kampuni itakayotisha mkulima na safari hii pamba itanunuliwa kupitia Amcos’’.

 

Katika hatua nyingine simalenga amewataka wananchi kuacha mara moja tabia ya kuchanganya mazao kwenye shamba moja wakati wa kilimo hali ambayo inawakosesha mavuno.

 

Amewasisitiza kutochanganya mazao ili kila zao lijitegemee ili waweze kupata mavuno yenye tija kuliko kuchanganya pamba, mbaazi, mahindi, choroko, maharage na ufuta kwenye ekari moja.

 

‘’Utaratibu mzuri ni kugawa sehemu ya shamba lako, eneo Fulani unalima pamba, kwengine unalima choroko…tusichanganye mazao kwa pamoja kwa sababu wadudu wanaoshambulia alizeti au mahindi wanashambulia pamba, hivyo pamba itengwe na isilimwe pamoja’’ amesisitiza Simalenga.

 

Awali wakulima wa pamba waliiomba serikali kuongeza bei ya pamba ili waweze kuwanufaisha, kuliko ilivyo sasa ambapo wanauza pamba kwa shilingi 1,150 kwa kilo moja.

 

MWISHO.

 

 

MKUU wa Wilaya ya Bariadi Simon Simalenga akiongea kwenye Mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Mwamlapa kata ya Kasoli wilayani humo kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi.


Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Simon Simalenga (Kushoto) akiwasilikiza wananchi waliojitokeza kuwasilisha kero mbalimbali katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Mwamlapa kata ya Kasoli.


Mamia ya Wananchi waliojitokea kumsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Simon Simalenga (wa pili kulia jukwaani) kwenye mkutano ulifanyika kijiji cha Mwamlapa kata ya Kasoli.


 Zao la pamba likiwa shambani.

 

 

 

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post