Serikali yasimamisha Uchenjuaji Madini Dutwa namba 2.

Mgodi wa Dutwa namba mbili (EMJ) unaosadikiwa kutiririsha maji yenye sumu.
  

 

Na COSTANTINE MATHIAS, Busega.

 

BAADA ya Wananchi wa Kijiji cha Imalamate wilayani Busega Mkoani Simiyu, kulalamikia mgodi wa Dutwa namba 2 kutiririsha maji yanayosadikiwa kuwa na sumu, serikali imefunga shughuli za uchenjuaji na uzalishaji katika mgodi huo.

 

Akizungumza mara baada ya kutembelea eneo hilo, Mkuu wa wilaya hiyo Faidha Salum amewataka wananchi kuwa na subira wakati serikali kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) wakichunguza madhara ya maji hayo kwa binadamu na wanyama.

 

Amesema serikali imeshaagiza uchanjuaji wa madini katika mgodi huo usimame kutokana na kuzalisha maji yenye kemikali nyingi ambayo yanaathiri mifugo na viumbe wengine.

 

‘’ndani ya wiki mbili au tatu tutakuwa na majibu, vipimo vya maji siyo kama malaria, ni sampo mbalimbali na wataenda maabara kujiridhisha na baada tutarudi kukaa pamoja’’ amesema na kuongeza.

 

‘’Kwa sasa hivi tumeshaagiza uchenjuaji usimamishwe, uchenjuaji wa madini tunasimamisha kwa muda sababu unaleta maji yenye kemikali nyingi ambayo yanaathiri wananchi na viumbe waliko kwenye maeneo yetu’’.

 

Ameongeza kuwa siku ya jumatano (June 5, 2024) watakutana na wamiliki na waendeshaji wa mradi huo, wataalamu wa madini, mazingira, ofisi ya Mkuu wa wilaya na Mkurugenzi ili kujadili kwa pamoja namna ya kumaliza tatizo hilo.

 

Ameongeza kuwa serikali itahakikisha inasimamia makubaliano na utaratibu ambao hautaathiri upande wowote ikiwemo kudhibiti maji yanayotiririka kuelekea kwenye maeneo ya wananchi.

 

‘’Msitumie maji haya, wale watoto wanaochunga ng’ombe, wasitumie maji kwa muda huu…athari yake tumeiona ikiwemo samaki kufa, niwaombe sana viongozi wenzangu tusaidiane’’ ameseam Faidha.

 

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa wilaya amewahakikishia wananchi wa Imalamate kuwa katika mradi wowote ndani ya wilaya hiyo, wazawa watapewa kipaumbele kwenye ajira kuliko wageni.

 

Amesema watahakiki watumishi walioko katika mgodi wa huo ili kujiridhisha wananchi wangapi wa Imalamate (Busega) wameajiriwa katika mgodi huo sababu kuna shughuli zingine hazihitaji taaluma.

 

MWISHO.

 

Samaki wakiwa wamekufa kutokana na kutiririshiwa maji yanayosadikiwa kuwa na sumu.

 

Samaki wakiwa wamekufa kutokana na kutiririshiwa maji yanayosadikiwa kuwa na sumu.


Mkuu wa wilaya ya Busega, Mkoani Simiyu Faidha Salum, akiongea na wananchi wa kijiji cha Imalamate kuhusiana na mgodi wa Dutwa namba 2 (EMJ) kutiririsha maji yanayosadikiwa kuwa na sumu.
 
 
 
 
 

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post