Na
Derick Milton, Maswa.
Walimu katika Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu wamesema
kuwa mfumo wa huduma binafsi kwa wafanyakazi (ESS) itakuwa suruhisho sahihi
kwao na wafanyakazi wengine wa serikali ambao wamekuwa wakiteseka na mikopo
umiza.
Wamesema kuwa mfumo huo unamwezesha mwalimu kuomba
mkopo akiwa shuleni kwa kutumia simu, lakini pia ni mfumo ambao unaongeza usiri
kwa mkopaji ikiwa pamoja na kupata mkopo kwa haraka.
Walimu hao wamesema hayo jana, wakati wa kongamano la
siku ya mwalimu lililoandaliwa na Benki ya NMB (Mwalimu Spesho) ambapo zaidi ya
walimu 200 walishiriki kongamano hilo linalolenga kutoa masuruhisho kwa
mwalimu.
Walisema mikopo umiza licha ya kuwaumiza katika
urejeshaji pamoja na riba kubwa, kitendo cha mwalimu kupata mkopo kwa haraka na
kuweza kutatua matatizo yake kwa haraka kimekuwa kichocheo kikubwa kwao
kuikimbilia.
“ Wengi tunakimbilia mikopo umiza, maana ukiomba leo
mkopo unapewa kesho, ni haraka sana mwalimu kuhudumiwa, tofauti na huku kwenye
benki ambapo inamchukua mtu wiki moja au mbili kupata huduma,” alisema Mshua
Msuluja Mwalimu.
Hata hivyo walimu hao wamesema kuwa baada ya kupewa
elimu na NMB juu ya mfumo huo kupitia kongamano hilo, wamesema walimu wengi
hawatendelea kukimbilia mikopo umiza.
“ Tunaishukuru NMB kutupatia elimu hii, kwanza tumeona
kuna usiri kutumia mfumo huu, yaani ni wewe mwalimu na Afisa utumishi tu, siyo
kama zamani ambapo mwalimu ilikulazimu kuzunguka na fomu halmashauri kila mtu
anakuona,” Alisema Mwalimu Spora Kweka.
Akizungumza mara baada ya kongamano hilo Meneja
Mwandamizi Idara ya wateja Binafsi benki ya NMB Queen Kinyamagoha alisema NMB
kama taasisi kinara wa fedha nchini imekuwa na utaratibu wa kukutana na walimu
na kuwapa masuruhisho kifedha.
Alisema kupitia kongamano hilo walimu wamefundishwa
jinsi ya kutumia mfumo mpya wa ESS wa kupata mkopo kutoka katika taasisi za
kifedha ikiwemo NMB, mfumo ambao unawaweza kupata huduma hiyo akiwa nyumbani.
“ tunatambua kuwa walimu kazi yao kubwa ni kufundisha
watoto, kupitia mfumo huu anaweza kupata mkopo hata kama yupo shuleni
anafundisha kwa kutumia simu yake, hii itampunguzia usumbufu na kupoteza muda,”
alisema Kinyamagoha.
Awali akizungumza katika kongamano hilo, Meneja wa NMB
Kanda ya Magharibi Restus Essenga alisema kuwa benki hiyo imeboresha huduma ya
mikopo kwa walimu ambapo awali walikuwa wanaweza kukopa kwa muda wa miaka 5
hadi 8 lakini muda umeongezwa hadi miaka 10.
“ Lengo la kuongeza muda tunataka huyu Mwalimu aweze
kukopa kiasi kikubwa cha fedha ambacho kitaweza kumwezesha kufanya shughuli
zake kikamilifu na kuweza kufikia malengo ambayo amejiwekea,” alisema Essenga.
Post a Comment