Walimu Maswa waipongeza NMB Elimu mfumo wa ESS.

Afisa Mahusiano Benki ya NMB Wilayani Maswa Mkoani Simiyu Deusdeth Mush akizungumza mbele ya walimu wa Wilaya hiyo, wakati wa kongamano la siku ya Mwalimu Wilayani humo, lililoandaliwa na Benki ya NMB.

Meneja Benki ya NMB Kanda ya Magharibi Restus Essenga akizungumza na walimu wa Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu (hawapo pichani) wakati wa kongamano la siku ya Mwalimu lililoandaliwa na Benki hiyo Wilayani humo.






Na Derick Milton, Maswa.


Walimu katika Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu wamesema kuwa mfumo wa huduma binafsi kwa wafanyakazi (ESS) itakuwa suruhisho sahihi kwao na wafanyakazi wengine wa serikali ambao wamekuwa wakiteseka na mikopo umiza.


Wamesema kuwa mfumo huo unamwezesha mwalimu kuomba mkopo akiwa shuleni kwa kutumia simu, lakini pia ni mfumo ambao unaongeza usiri kwa mkopaji ikiwa pamoja na kupata mkopo kwa haraka.


Walimu hao wamesema hayo jana, wakati wa kongamano la siku ya mwalimu lililoandaliwa na Benki ya NMB (Mwalimu Spesho) ambapo zaidi ya walimu 200 walishiriki kongamano hilo linalolenga kutoa masuruhisho kwa mwalimu.


Walisema mikopo umiza licha ya kuwaumiza katika urejeshaji pamoja na riba kubwa, kitendo cha mwalimu kupata mkopo kwa haraka na kuweza kutatua matatizo yake kwa haraka kimekuwa kichocheo kikubwa kwao kuikimbilia.


“ Wengi tunakimbilia mikopo umiza, maana ukiomba leo mkopo unapewa kesho, ni haraka sana mwalimu kuhudumiwa, tofauti na huku kwenye benki ambapo inamchukua mtu wiki moja au mbili kupata huduma,” alisema Mshua Msuluja Mwalimu.


Hata hivyo walimu hao wamesema kuwa baada ya kupewa elimu na NMB juu ya mfumo huo kupitia kongamano hilo, wamesema walimu wengi hawatendelea kukimbilia mikopo umiza.


“ Tunaishukuru NMB kutupatia elimu hii, kwanza tumeona kuna usiri kutumia mfumo huu, yaani ni wewe mwalimu na Afisa utumishi tu, siyo kama zamani ambapo mwalimu ilikulazimu kuzunguka na fomu halmashauri kila mtu anakuona,” Alisema Mwalimu Spora Kweka.


Akizungumza mara baada ya kongamano hilo Meneja Mwandamizi Idara ya wateja Binafsi benki ya NMB Queen Kinyamagoha alisema NMB kama taasisi kinara wa fedha nchini imekuwa na utaratibu wa kukutana na walimu na kuwapa masuruhisho kifedha.


Alisema kupitia kongamano hilo walimu wamefundishwa jinsi ya kutumia mfumo mpya wa ESS wa kupata mkopo kutoka katika taasisi za kifedha ikiwemo NMB, mfumo ambao unawaweza kupata huduma hiyo akiwa nyumbani.


“ tunatambua kuwa walimu kazi yao kubwa ni kufundisha watoto, kupitia mfumo huu anaweza kupata mkopo hata kama yupo shuleni anafundisha kwa kutumia simu yake, hii itampunguzia usumbufu na kupoteza muda,” alisema Kinyamagoha.


Awali akizungumza katika kongamano hilo, Meneja wa NMB Kanda ya Magharibi Restus Essenga alisema kuwa benki hiyo imeboresha huduma ya mikopo kwa walimu ambapo awali walikuwa wanaweza kukopa kwa muda wa miaka 5 hadi 8 lakini muda umeongezwa hadi miaka 10.


“ Lengo la kuongeza muda tunataka huyu Mwalimu aweze kukopa kiasi kikubwa cha fedha ambacho kitaweza kumwezesha kufanya shughuli zake kikamilifu na kuweza kufikia malengo ambayo amejiwekea,” alisema Essenga.

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم