Kilogramu 1,066.105 Za Dawa za Kulevya Zakamatwa

 

Dar es Salaam, Novemba 12, 2024

 

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanya operesheni katika maeneo mbalimbali nchini kati ya Oktoba na Novemba 2024, na kufanikiwa kukamata kilogramu 1,066.105 za dawa za kulevya, mililita 447 za dawa tiba zenye asili ya kulevya, na kuteketeza jumla ya ekari 157.4 za mashamba ya bangi na lita 19,804 za kemikali bashirifu, huku watuhumiwa 58 wakikamatwa katika operesheni hizo.

Kati ya dawa hizo, kilogramu 687.32 za skanka na kilogramu moja (01) ya hashishi zilikamatwa eneo la Goba, Dar es Salaam, zikiwa zimefichwa ndani ya nyumba ya mtuhumiwa. Uchunguzi umebaini kuwa wateja wengi wa skanka ni wanawake, ambao hudai kutumia dawa hizo  kupunguza msongo wa mawazo na kujistarehesha. Skanka ni aina ya bangi yenye kiwango kikubwa cha sumu, inavyosababisha madhara makubwa kiafya. Vilevile, hashishi ambayo hutengenezwa kwa mchanganyiko wa maua na mafuta ya mbegu za bangi, inapovutwa huzalisha kemikali hatari zinazoweza kusababisha magonjwa ya akili kwa haraka. Mara nyingi jamii huamini kuwa watu wanaopatwa na magonjwa haya wamerogwa.

Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Mamlaka ilikamata mililita 120 za dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Codein, zikiwa zinasafirishwa kwenda nje ya nchi, pamoja na mililita 327 zilizokutwa nyumbani kwa mtuhumiwa eneo la Tabata Kinyerezi. Dawa hizo ziliingizwa nchini kinyume na taratibu, zikiwa zimewekwa chapa bandia ya dawa za kuogeshea mbwa na paka ili kuepuka kubainika. Kukamatwa kwa dawa hizi ni ishara ya uwepo wa tatizo la matumizi holela ya dawa za tiba zenye asili ya kulevya, Hali hii inachangiwa na kuimarika kwa udhibiti  wa dawa za kulevya na kusababisha wafanyabiashara na watumiaji kutumia dawa tiba ya kulevya kama mbadala wa dawa za kulevya.

Mkoani Dodoma, Mamlaka imewakamata watuhumiwa wawili Suleiman Mbaruku Suleiman (maarufu Nyanda), mwenye umri wa miaka 52, na Kimwaga Msobi Lazaro (miaka 37) wakazi wa mtaa wa Kinyali, kata ya Viwandani. Watuhumiwa hao walikamatwa na jumla ya gramu 393 za heroin. Nyanda anafahamika kama kinara wa biashara ya dawa za kulevya mkoani humo na amekuwa akifuatiliwa kwa muda mrefu.

Kupitia operesheni za kanda, DCEA pia imekamata kilo 303.553 za bangi, gramu 103.8 za heroin, na kilo 63 za mirungi katika maeneo mbalimbali nchini.

Mafanikio haya ni matokeo ya nia thabiti ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha kuwa tatizo la dawa za kulevya linakomeshwa ili kulinda afya na usalama wa watanzania.

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inawaomba wananchi waendelee kuunga mkono jitihada hizi kwa kufichua wafanyabiashara wa dawa za kulevya na kuhamasishana kutoshiriki katika biashara na matumizi ya dawa za kulevya

Imetolewa na,

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali

MAMLAKA YA KUDHIBITI NA KUPAMBANA  NA DAWA ZA KULEVYA.


Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post