Kamati ya Bunge TAMISEMI yawataka Watumishi kuzingatia Ubora katika Utoaji wa Huduma.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Denis Londo (anayeandika) akipata maelezo wakati akikagua wodi ya wanawake katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Bariadi Khalid Mbwana.
 


Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) wakiongea na wakina mama waliofika kwenye hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi iliyoko Dutwa kwa ajili ya kupata huduma ya chanjo kwa watoto wao.


Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) wakiongea na wakina mama waliofika kwenye hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi iliyoko Dutwa kwa ajili ya kupata huduma ya chanjo kwa watoto wao.

 

 

Naibu Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Deogratius Ndejembi (mwenye shati la kaki) akitoa salama za Rais Samia kwa akina mama waliofika kweny Hospitali ya Halmashauri ya wilaya ya Bariadi-Dutwa kwa ajili ya kupata huduma ya chanjo kwa watoto wao, kulia ni Katibu Tawala wilaya ya Bariadi Nichodemus Shirima, mwenye shati jeupe ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dk. Yahaya Nawanda.


 

Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.

 

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imezitaka Halmashauri kote nchini kuhakikisha zinaboresha haiba ya Watumishi wa Umma ili kuendana na utoaji wa huduma kwa wananchi.

 

Imesema Watumishi wa Umma ndiyo haiba ya serikali kwa wananchi, na kwamba serikali inaleta fedha nyingi katika kuboresha huduma za maendeleo, hivyo ni jukumu la watendaji kutoa huduma zinazofanana na uwekezaji wa serikali.

 

Hayo yamebainishwa leo na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Denis Londo mara baada ya kukagua ujenzi wa Jengo la dharura, Wodi ya Wanawake na Wanaume pamoja na jengo la Upasuaji katika hospitali ya Halmashauri ya wilaya ya Bariadi iliyopo Dutwa.

 

Mwenyekiti huyo amesema ni muhimu mapato ya ndani yakaenda kukamilisha mahitaji madogomadogo ikiwemo njia za watembea kwa miguu katika hospitali hiyo.

 

‘’Rais Samia amejitahidi sana katika kipindi hiki kushusha fedha katika ngazi ya kijiji, Kata, Wilaya na Mkoa…tuboreshe sana haiba ya watendaji wetu kwa wananchi, ili waendane na thamani ya fedha zilizowekezwa’’ amesema.

 

Aliwataka watendaji wa serikali kujikita kusimamia ukusanyaji wa mapato na kuona yanaleta tija kwa wananchi, kwa sababu pia mapato ya ndani yanawajibu wa kuboresha huduma za wananchi ambao ni walipa kodi wa mapato ya ndani.

 

Kwa upande wake Naibu Waziri TAMISEMI Deogratius Ndejembi amesema Rais Samia Suluhu Hassan alihakikisha anatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za wilaya na vituo vya afya ili kuwasogezea huduma wananchi karibu na maeneo yao.

 

Amesema katika mwaka wa fedha ujao wataomba fedha za kujenga nyumba 300 za watumishi wa afya nchi nzima huku akiongeza kuwa fedha zilizokuwa zinapelekwa kwenye Halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa majengo kwenye Hospitali zilikuwa hazitoshi.

 

‘’kwenye maeneo yenye changamoto, tutahakukisha tunaongeza vifaa tiba vinavyoendana na eneo husika…hapa kuna Bil. 3.9 zimeletwa kwa majengo ya hospitali, njia za kutembelea zinatakiwa kujengwa kwa mapato ya ndani, sababu serikali imeshawatua mzigo, huwezi kuwa na jengo la upasuaji bila njia ya kutembelea kwenda wodini’’ amesema Ndejembi.

 

Ameongeza kuwa ifikapo jumatatu atahahikisha wataalamu wa vifaa kwenye jengo la dharura wamefika kwa ajili ya kutoa mafunzo ili utoaji wa huduma uweze kuanza.

 

Awali Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dk. Yahaya Nawanda amesema Hospitali ya Wilaya ya Bariadi ilipokea kiasi cha shilingi bil. 3.4 kwa ajili ya kutekeleza ujenzi wa majengo 16.

 

Amesema fedha hizo zilipokelewa kwa awamu mbalimbali na kwamba ujenzi wa majengo hayo umekamilika na huduma za matibabu zimeanza kutolewa kwa wananchi.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Khalid Mbwana amesema walipokea kiasi cha shilingi milioni 800 kwa ajili ya ujenzi wa majengo manne.

 

‘’Tumejenga wodi ya wanaume na wanawake, jengo la upasuaji pamoja na jengo la kuhifadhia maiti, tulipokea pia mil. 390 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya watumishi (three in one) pamoja na ujenzi wa jengo la dharura’’ amesema Mbwana.

 

MWISHO.

 

 Naibu Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Deogratius Ndejembi (mwenye shati la kaki) akitoa salama za Rais Samia kwa akina mama waliofika kweny Hospitali ya Halmashauri ya wilaya ya Bariadi-Dutwa kwa ajili ya kupata huduma ya chanjo kwa watoto wao.

 

Jengo la Upasuaji katika Hospitali ya Halmashauri ya wilaya ya Bariadi iliyoko Dutwa ambalo limekamilika kujengwa.


Vitanda vya kutumia umeme katika jengo la dharura lililoko Hospitali ya Wilaya ya Bariadi iliyoko Dutwa.
 
 
Baadhi ya vifaa tiba katika Hospitali ya wilaya ya Bariadi iliyoko Dutwa.


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Denis Londo (wa kwanza kulia) akikagua sehemu za vifaa tiba katika hospitali ya Wilaya ya Bariadi, wa pili kulia ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dk. Flavian Jacobo.
 

 Jengo la Dharura (EMD) katika Hospitali ya wilaya ya Bariadi iliyoko Dutwa.

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post