Na Derick Milton, Kahama.
Wateja wa Benki
ya NMB wameendelea kujipatia zawadi mbalimbali zinazotolewa na beki hiyo
kupitia kampeini yake ya Bonge la Mpango, ambapo jana Bernad Kimario mkazi wa
Kahama Mkoani Shinyanga amekabidhiwa trekta ya kilimo (Powertiller) baada ya
kuibuka mshindi.
Hafla ya kukabidhi
zawadi hiyo imefanyika mjini Kahama, ambapo mbali na mshindi huyo Benki hiyo
ilimzawadia jiko la umeme Chausiku Tindiga mkazi wa Shinyanga ambaye aliibuka
mshindi wa pili kwenye kampeini hiyo.
Wateja hao
waliibuka washindi katika droo hiyo iliyochezeshwa na Benki hiyo katika wiki ya
nane ya kampeini hiyo, ambapo walikabidhiwa zawadi hizo na Meneja wa NMB Kanda
ya Magharibi Restus Assenga.
Mbali na kukabidhi
zawadi hizo, Benki hiyo iliendesha droo ya kumi ya kampeini hiyo ambapo Kalinga Hassan kutoka mkoani Mwanza, alibuka
mshindi wa kwanza na kujishindia zawadi ya trekta ya kilimo (Powertiller).
Droo hiyo ambayo iliendeshwa na Meneja mauzo
NMB Janeth Nyamko, ilimtangaza pia Fadhili Mwanjegwa kuwa mshindi wa pili
ambapo alijishindia zawadi ya pikipiki ya magurudumu matatu (Guta).
Akizungumza mara baada ya zoezi hilo,
Meneja wa Kanda Assenga alisema kuwa kampeini hiyo inalenga kuhamasisha
watanzania na wateja wa NMB kuwa na utamaduni wa kujiwekea akiba ili kuweza
kukabiliana na dharura mbalimbali.
Alisema kuwa NMB inaamini kuwa watu
wakijenga tabia ya kujiwekea kwenye akaunti zao wataweza kujiepusha na mikopo
umiza, au kausha damu pindi wanapopata dharura inayohitaji fedha.
“ Tunawasisitiza zaidi wateja wetu wa NMB
kujitokeza kwa wingi kushiriki kampeini hii ambayo inaendelea, wachangamkie
fursa hii, watu wameshinda pesa taslimu, majiko ya umeme, trekta za kilimo,
pikipiki, pamoja na TV janja,” alisema Assenga.
Alisema tangu kampeini hiyo imeanza jumla
ya washindi 64 wamejishindia pesa taslimu, ambapo 60 kati ya hao wamejipatia
kiasi cha Shilingi Laki moja (100,000) kila mmoja na washindi wanne wamejipatia
Milioni tano kila mmoja.
Kwa upande wake Bernad Kimario mara baada
ya kupatiwa zawadi ya trekta ya kilimo (Powertiller) alisema kuwa mwanzoni
wakati anapigiwa simu kuwa ameshinda alihisi kuwa ni uongo au anataka
kutapeliwa.
Alisema kuwa aliamua kwenda katika tawi
la benki ya NMB kuulizia kama ni kweli, ndipo alipokutana na jina lake na
kugundua kuwa Kampeini hiyo siyo uongo wala utapeli bali ni ukweli hivyo watu
wajiwekee akiba ili waweze kushinda.
“ Nashukuru sana kwa nyenzo hii ambapo
NMB imenipatia, sikutumia nguvu kubwa kuipata, ni kujiwekea akiba kwenye
akaunti yangu, nawasisitiza watu washiriki, hii trekta itanisaidia sana kwenye
kilimo changu cha mahindi na mchele,” alisema Kimario.
MWISHO.
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com
Post a Comment