Matrekta ya Kunyunyizia na Kudhibiti Wadudu wa Pamba yafanyiwa Majaribio Kishapu.

 

TREKTA lililotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Kilimo chini ya Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), likifanya majaribio ya kunyunyizia shamba la Mkulima wa Pamba katika Kijiji Cha Mwanulu wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga.


Na COSTANTINE MATHIAS, Kishapu-Shinyanga.


KWA mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, Wizara ya Kilimo kupitia Bodi ya Pamba nchini (TCB), imeingiza nchini Teknolojia mpya ya Matrekta yatakayotumika kunyunyizia dawa na kudhibiti wadudu wanaoshambulia zao la pamba, kwa lengo la kurahisisha upuliziaji katika mashamba makubwa ya wakulima nchini.


Katika Majaribio ya Teknolojia hiyo, Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga, Wakulima wa Pamba wameipongeza serikali kwa kuendelea kusambaza Teknolojia ambazo zinarahisisha shughuli za kilimo, Upandaji na upuliziaji kwa lengo la kudhibiti wadudu wanaofyonza na kutafuna vitumba vya Pamba shambani.


Alexander Malelemba na Mandu Magima, wakulima wa Kijiji Cha Mwanulu wilayani humo wamesema awali Wakulima hawakuwa na Elimu ya Upandaji na upuliziaji, lakini baada ya kupatiwa Elimu kupitia Maafisa Ugani wa BBT wamebadilika na wanatarajia kuzalisha kwa tija.


Mhandisi James Kisinza Ndimu kutoka Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), amesema kwa muda mrefu wamekuwa wakisaidia wakulima wa Pamba kuwapa zana nzuri ambazo zinasaidia kuinia Kilimo chao ili kuongeza toja.


Kisinza amesema awali walianza na pampu zaidi ya 100,000 ambazo zimegawiwa kwa wakulima wa Pamba nchi nzima, lakini kutokana na mabadiliko ya Sayansi Bodi hiyo ilinunua ndege nyuki katika msimu 2024/2025 ambazo zimesaidia kunyunyizia madawa katika mashamba ya wakulima.


"Mwaka huu tumeongeza Mitambo ya Matrekta 16 kwa ajili ya upuliziaji katika wilaya ya Kishapu, tuko shambani tunafanya majaribio...serikali kupitia Wizara ya Kilimo itawezesha wakulima wetu kufikia Malengo yao" amesema.


Amesema mashine hiyo inarahisha kazi ambapo kwenye ekari moja inaweza kutumia dakika tano na kwamba inawalenga wakulima wenye mashamba makubwa yaliyopandwa kitaalamu lakini huduma hiyo inawafikia wakulima bure bila malipo yoyote.


Ameongeza kuwa Mpango wa serikali ni kuongeza matumizi ya Teknolojia hasa kwa wilaya za kimkakati zenye uzalishaji Mkubwa wa zao la Pamba ikiwemo Kishapu (Shinyanga), wilaya za Mkoa wa Simiyu (Bariadi, Maswa, Meatu, Itilima), Bunda (Mara) na Mkoa wa Katavi.


Mratibu wa zao la Pamba wilaya ya Kishapu Richard Mangua ameipongeza serikali ya Dk. Samia kupitia Wizara ya Kilimo ambapo wameweza kuwafikia wakulima 52,000 ambao wamesajiliwa ili kupatiwa huduma za Ugani.


Amesema wakulima wamefuata kanuni za kilimo na hali ya mashamba ni nzuri na kwamba wamepata Mitambo mipya itakayorahisisha zoezi la kudhibiti wadudu wanaoshambulia zao la Pamba.


Mratibu huyo amesema katika msimu wa 2023/2024 walizalisha tani mil.30,  mwaka 2024/2025 walizalisha tani mil. 20 na Mwaka huu 2025/2026 wanatarajia kuzalisha kilo mil.50.

Aidha, Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuipa kipaumbele sekta ya Kilimo kupitia zao la pamba kwa kusambaza Maafisa Ugani kupitia Mpango wa Jenga Kesho Bora (BBT), Matrekta kwa ajili ya kulima wakulima wa Pamba pamoja na kusambaza Teknolojia za Upuliziaji ikiwemo ndege nyuki, maboza na Matrekta ya kupulizia wa dawa ili kuongeza tija ya zao hilo.


Mwisho.



Mhandisi James Kisinza Ndimu kutoka Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), akiongea na waandishi wa Habari (hawapo pichani) wakati wa majaribio ya Trekta kwa ajili ya Unyunyiziaji wa wadudu wa Pamba wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga.


Matrekta yakiwa yamefungwa kwa ajili ya kufanyiwa majaribio ya kunyunyizia mashamba makubwa ya wakulima wa pamba.

Mratibu wa zao la Pamba wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Richard Mangua, akizungumzia Trekta lililotolewa na Serikali kwa ajili ya kunyunyizia mashamba makubwa ya wakulima wa Pamba.















Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post