Rc Kihongosi Amkabidhi Mkandarasi Kuchimba visima Kwa ajili ya Umwagiliaji.


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Kenan Kihongosi akimkabidhi nyaraka Mkandarasi kutoka kampuni ya MNFM Construction Ltd kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa kuchimba visima kwa ajili ya Umwagiliaji.


Na Mwandishi Wetu.


MKUU wa mkoa wa Simiyu, Kenan Kihongosi, amekabidhi kwa Mkandarasi mradi wa uchimbaji wa Visima kwa ajili ya kilimo cha Umwagiliaji kwenye Mtaa wa Gagabali kilichopo katika Kata ya Nyakabindi, Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani humo.


Akizungumza leo (Feb 18, 2025) na Wananchi  wakati wa kukabidhi mradi huo kwa mkandarasi, Kenan amewataka Wananchi  kutoa ushirikiano kwa mkandarasi kutoka kampuni ya MNFM Construction LTD.


Amewataka Wananchi kulinda mindombinu ya mradi huo ili uweze kuleta manufaa kwa Watu wote huku akisisitiza Mkandarasi  huyo kuhakikisha anakamilisha mradi huo ndani ya muda uliopangwa ili Wananchi waweze kunufaika.


Aidha amewataka Wataalamu wa Tume ya umwagiliaji  Mkoa wa Simiyu kuhakikisha Wanasimamia utekelezaji wa mradi huo ili uweze kukamilika kwa ubora na viwango vinavyotakiwa.


Ameuagiza Uongozi Wilayani Bariadi kusimamia uundwaji wa chama cha wakulima wa Umwagiliaji katika Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ili chama hicho kiwajibike katika utunzaji wa mradi. 

 

Awali akiwasilisha Taarifa ya mradi huo, Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoa  wa Simiyu, Jeremiah Seme amesema utekelezaji wa mradi huo unaogharimu zaidi ya shilingi Mil. 139   ni  maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyeagiza kuanzishwa kwa mradi wa Uchimbaji visima katika eneo hilo ambapo zaidi ya Ekari 160 zitanufaika na mradi huo.


Amesema mradi huo utatekelezwa kwa muda wa siku 180 ukihusisha uchimbaji wa Visima 4 katika Halmashauri 4 za Mkoa wa Simiyu.


Akizungumza na Wananchi katika Mtaa wa Gagabali, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nyakabindi Elias Masanja amesema  Mradi huo utasaidia Wananchi wa Gagabali Wilayani Bariadi kufanya kilimo cha umwagiliaji kwa uhakika zaidi.


Mwisho.







Wananchi kutoka Kata ya Nyakabindi, Halmashauri ya Mji wa Bariadi ambao wameshiriki sehemu ya makabidhiano ya Mkandarasi atakayetekeleza uchimbaji wa Visima virefu kwa ajili ya Umwagiliaji.




Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم