.
Na COSTANTINE MATHIAS, Meatu-Simiyu.
WAKULIMA
wa Pamba kutoka Kijiji cha Mwambiti kata ya Mwamishali wilayani Meatu
Mkoani Simiyu wameanza kunufaika na Elimu ya Mbolea hai wanayotengeneza
wenyewe kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa zao la Pamba.
Mbolea
hiyo ambayo inatengenezwa kutoka na malighafi za Asili zinazotokana na
masalia ya viumbe hai ikiwemo Majibu, kinyesi cha ng'ombe ma mkaa na
kwamba mbolea hiyo imesheheni virutubisho vitatu ambavyo ni Nitrojeni,
Phosiforasi na Potasium.
Akizungumza
wakati wa Uandaaji wa mbolea hiyo, Afisa Kilimo kupitia Mpango wa Jenga
Kesho Bora (BBT) katika Kijiji cha Mwambiti, Salome Mathias amesema
malighafi za mbolea hiyo hupatikana karibu na makazi ya wakulima, hivyo
ni rahisi kutengeneza na haina gharama.
Amesema mbolea hiyo ya Asili haina kemikali tofauti na mbolea za viwandani ambazo huharibu udongo na mazingira kwa ujumla.
"Mbolea
hii imegundulika na imesaidia kuongeza uzalishaji na tija katika zao la
Pamba tofauti na mbolea za madukani...katika majaribio ya msimu
uliopita tulitengeneza mapipa 42 na kusambazwa kwa wakulima zaidi ya 300
ambapo ilileta natokea chanya na mimea iliyopuliziwa ilikuwa na vitumba
60 mpaka 100" amesema.
Ameeleza
kuwa wakulima waliotumia mbolea hiyo, wamevuna kilo 800, 900 mpaka 1200
kwa ekari moja na kabla ya mbolea hai wakulima walikuwa wanavuna kilo
200, 250 mpaka 300.
Amemshukuru
Bodi ya Pamba Tanzania kwa kuwaletea mbolea hiyo mapema kabisa na
inatumika katika Kilimo cha zao la Pamba hai na Pamba ya kawaida kwa
sababu pia inadhibiti wadudu na kurutubisha udongo.
Afisa
Kilimo kutoka Bodi ya Pamba Tanzania, Edward Nyawile amesema mbolea hai
ilianza kufanyiwa majaribio katika msimu wa 2023/2024 katika wilaya za
Igunga, Meatu, Bunda, Butiama na Kishapu.
Amesema
mbolea hiyo imeonyesha tija kwa Wakulima ambao wamefanyiwa majaribio
kwa kuongeza uzalishaji kutoka kilo 200 kwa ekari na baada ya kutumia
mbolea hao waliipata kilo 800 mpaka 1000 kwa ekari moja.
"Bodi
ya Pamba imeona mbolea hai itasaidia wakulima kuongeza tija na
uzalishaji katika zao la Pamba, msimu wa 2024/2025 matumizi ya mbolea
hai yamelengwa katika wilaya ya Meatu kutoka na kuwa kinara wa
uzalishaji wa Pamba hai" amesema.
Amesema
wanatarajia kutengeneza lita 400,000 za mbolea hai zitakazosambazwa kwa
wakulima wa wilaya ya Meatu katika msimu huu na pia kuna wilaya
zinaendelea kunufaika na msimu ujao wanatarajia kusambaza lita Mil. 7 za
mbolea hai nchi nzima.
Bule
Nyolobi, mkulima wa zao la Pamba katika Kijiji cha Mwambiti amesema
amepata Mafanikio makubwa ya kuongeza uzalishaji kutokana na kutumia
mbolea hai tofauti na awali ambapo alikuwa anapata mavuno haba.
Rhoda Masanja, mkazi na mkulima wa Kijiji cha Mwambiti amesema mbolea hiyo imeongeza mavuno kutoka kuzalisha kilo 300 kwa ekari moja na kufikia kilo 800 mpaka 1000 kwa ekari moja.
Mwisho.
إرسال تعليق