MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa (CCM) Abdulkadri Mushi (katikati) akiongoza wajumbe wa kamati ya siasa ya mkoa Kigoma kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa shule ya sekondari Ruhuli wilayani Kakonko.
Na Fadhili Abdallah.
KIASI cha Shilingi Milioni 603.8 zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari Ruhulu wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma zinaelezwa kuondoa adha ya wanafunzi wa shule ya msingi kijijini hapo wanaofaulu masomo yao kwa ajili ya kujiiunga na kidato cha kwanza kutembea umbali wa kilometa 25 kwa ajili ya kupata elimu ya sekondari
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Kakonno, Stephano Ndaki alisema hayo mbele ya Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Taifa ya CCM,Abdulkadri Mushi anayefanya ziara kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo ya wilaya hiyo akiongoza wajumbe wa kamati ya siasa ya CCM mkoa Kigoma.
Stephano Ndaki, Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya Kakonko.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa hadi sasa Vyumba nane vya madarasa, jengo la utawala, maabara tatu, chumba cha maktaba na chumba cha TEHAMA na vyoo vya wasichana na wavulana vimekamilika ambapo mradi huo umetekelezwa kupitia mpango wa uboreshaji wa shule za sekondari nchini (SEQUIP) na kwamba mradi upo kwenye hatua za ukamilishaji na shule inatarajia kuanza kuchukua wanafunzi kuanzia mwezi Machi mwaka huu.
Baadhi ya wananchi wa kata ya Muhange halmashauri ya wilaya Kakonko mkoani Kigoma akiwemo Felister Ndihululumiye amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa shule ya sekondari katika kata hiyo wakieleza kuwa imewatoa watoto wao katika mateso ya kutembea umbali mrefu kufuata masomo.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Muhange, Ibrahim Katunzi alisema kuwa awali kata hiyo ilikuwa na shule moja ya sekondari ya Ndalichako iliyopo kata kijiji cha Muhange lakini bado kumekuwa na umbali mrefu kwa wananchi kutoka kijiji cha Ruhuli wanaochaguliwa kujiunga na shule ya Ndalichako hivyo wengi wao ilikuwa kazi kubwa kwenda shule na utoro ulikuwa ni mkubwa.
Diwani wa kata ya Muhange Ibrahim Katunzi.
Akihitimisha ziara yake kwa kutembelea na kukagua mradi huo Mjumbe wa halmashauri kuu ya Taifa ya CCM, Abdulkadri Mushi amepongeza utekelezaji wa mradi huo kwamba umezingatia viwango lakini pia umetekelezwa ili kuweka mazingira wezeshi ya wanafunzi kupata elimu.
Mushi alisema kuwa kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan inaacha alama kwani kuondoa changamoto ya wanafunzi kutembelea umbali wa kilometa 50 kila siku kwenda shule na kurudi siyo ya jambo la kawaida hivyo shule hiyo itawezesha wanafunzi wengi kupenda masomo lakini pia itachangia kuongeza taaluma kwa wanafunzi watakaosoma shuleni hapo.
Mwisho.
Felister Ndalulumiye mwananchi wa kijiji cha Ruhulu wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma.
إرسال تعليق