Na Andrew Chale, Dar.

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, (Mb) anatarajiwa kuwa mgeni katika matembezi ya miaka 50 ya Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) yatakayofanyika saa 12:00 Alfajli hadi sasa 2:00 Asubuhi, 7 Machi 2025 eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hadi Mwenge ofisi za TET Makao makuu.

Akizungumza na vyombo vya habari mapema leo 20 Februari, Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt. Aneth Anselmo Komba amesema kuwa maandalizi yanaendelea vizuri na amewaomba wadau kuendelea kujitokeza kuchangia na kushiriki katika matembezi hayo ya hisani yatakayokuwa ya Kilometa Tano (KM 5).

"Katika kuadhimisha miaka 50, TET itafanya shughuli mbalimbali zinazoendana na majukumu yake makuu. Aidha, kupitia maadhimisho haya, TET imeanzisha kampeni ya Kitabu kimoja kwa Mwanafunzi mmoja.

Lengo la kampeni hii ni kuunga mkono juhudi za Serikali za kuchapa na kusambaza Vitabu vya Kiada kuanzia ngazi ya Elimu ya Awali, Darasa la Kwanza hadi la Saba na Kidato cha Kwanza hadi cha Sita ili kufikia uwiano wa kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja yaani (1:1).

"Ili kufikia lengo hili, TET inawaalika wadau wote wa elimu nchini ikiwemo Serikali, Sekta binafsi, mashirika ya dini, mashirika ya kimataifa na watu binafsi katika kuchangia na kushiriki katika Matembezi hayo ya hisani hiyo 7 mwezi Machi 2025 tukiwa pamoja na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, viongozi mbalimbali wa Serikali na binafsi na wadau wote wa ndani na nje,

Tutaanza saa 12:00 Alfajli hadi saa 2:00 Asubuhi, kuanzia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam eneo la Maktaba mpya kupitia Chuo cha Maji, Mlimani City, Mwenge na kuishia Ofisi za TET hapa Makao Makuu Mwenge na baadaye yatafuatiwa na hafla ya uzinduzi wa sherehe za Miaka 50 ya TET itakayoanza saa 3:00 asubuhi katika viwanja vya TET Makao Makuu." Amesema Dkt. Aneth Komba.

Aidha, amesema gharama za kushiriki, wadau kwa wadau kujisajili na kuchangia TSH. 50,000 (Fulana) au TSH. 150,000 (Trakisuti).

"Fedha hizi zitaelekezwa moja kwa moja katika uchapaji na usambazaji wa Vitabu vya Kiada kwa wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari Tanzania Bara na Zanzibar.

Taratibu za kuchangia na kujisajili zimebainishwa katika mitandao ya kijamii ya TET ya X, instagram na facebook inayopatikana kwa anwani ya taasisiyaelimutanzania. "Karibu tutembee pamoja kufanikisha lengo la Kitabu Kimoja kwa Mwanafunzi Mmoja". Amesema Dkt. Aneth Komba.

Dkt. Aneth Komba amesema kuchangia kampeni ya kitabu Kimoja kwa Mwanafunzi Mmoja kwa kutumia namba ya malipo ya Serikali ambayo ni 994040118259. "Kampeni hii ni endelevu, michango imekwishaanza kupokelewa na itaendelea kupokelewa 

mpaka siku ya kilele cha maadhimisho hayo Mwezi Juni, 2025. Wadau wote mnaalikwa kuendelea kuchangia kwa kutumia namba hii ya malipo ya serikali." Amesema Dkt. Aneth Komba.