Na COSTANTINE MATHIAS, Simiyu.
KAMATI ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu imeonyesha kutoridhishwa na Ujenzi wa chuo cha Ufundi Stadi (VETA) inaotekelezwa kwa gharama ya shilingi Bil. 1.48 kwa awamu ya kwanza na Wizara ya Elimu wilaya ya Busega Mkoani humo ambapo ujenzi wake unasuasua.
Akizungumzia Ujenzi huo kwenye ziara ya Kamati ya Siasa, iliyoanza ziara hivi leo, Mkuu wa Mkoa huo, Kenan Kihongosi ameitaka Wizara ya Elimu kuwatambua na kuwashirikisha viongozi wa serikali ngazi ya wilaya ili waweze kusimamia na kufanikisha utekezaji wa miradi mbalimbali.
Amesema kuwa Mradi huo wa ujenzi wa VETA, una changamoto kubwa katika Utekelezaji wake, lakini ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Busega pamoja na Mkurugenzi wake wamekuwa wakichukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwakumbusha kwa maandishi juu ya Utekelezaji wake na Umuhimu wa Mradi huo lakini bado kuna shida kidogo.
"Wizara wanapoleta hii miradi, wajue kuna viongozi kama Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi kwenye eneo husika wanaopaswa kujua Utekelezaji wake ili waguswe zaidi na miradi hii...kwa sababu, hapa leo tunaulizana gharama ya jengo, hakuna anayejua zaidi ya Wizara" amesema na kuongeza.
''hii ni changamoto, kama fedha zimeletwa zaidi ya Mil. 429 lakini bado majengo hayajamakilika, Wizara ya Elimu Wana Wajibu wa kufanya...hapa kama Mkoa hatujaridhika na huu Mradi." Amesema Kenan.
Ameongeza kuwa changamoto zote zinazojitokeza ikiwemo nondo kuoza, zinaweza kusababisha majengo kubomoka na kuitaka Wizara ya Elimu kuhakikisha wanasaidia chuo hicho kukamilika kwa wakati kwani Rais Dk. Samia ameshatoa fedha, hivyo wanatakiwa kutimiza Wajibu ili majengo hayo yakamilike kwa wakati.
Katibu wa CCM Mkoa wa Simiyu, Eva Ndegeleki, amesema kuwa Mradi huo unasuasua licha ya kuwa ni Mradi muhimu kwa ajili ya Watoto ambao watajifunza utaalamu na ujuzi mbalimbali ili wajikimu na waendeleze maisha yao na Taifa kwa ujumla.
Amemtaka Mkuu huyo wa Mkoa, kushirikiana Chama ili waweze kuwasiliana na Wizara kwa ajili ya ukamilishaji wa Mradi huo, ili ifikapo mwezi Juni mwaka huu wananchi wawe na matumaini na waone Mradi huo ukikamilika la wakati.
Awali, akiwasilisha Taarifa ya Ujenzi wa Mradi huo, Afisa Uthibiti Ubora wa Shule wilaya ya Busega, William Thomas amesema lengo la Mradi huo ni kupata Wataalamu watakaosaidia nchi baada ya kuhitimu mafunzo ya vyuo, kuwajengea vijana ujuzi na uwezo wa kujiajiri pamoja kupunguza tatizo la ajira nchini.
Ameeleza kuwa Mradi huo utakuwa na majengo 18 ambapo awamu ya kwanza itahusisha majengo 09 na awamu ya pili majengo 9, na kwamba Mradi huo unatekelezwa kwa Force Account kwa gharama ya shilingi Bil. 1.48 kwa awamu ya kwanza na hadi sasa Shilingi Mil. 429 zimepokelewa.
"Jengo la Utawala limefikia asilima 50, madarasa yako asilima 50, kuna changamoto ya ukosefu wa nondo kwa ajili ya kufunga lenta, Nguzo za kunyanyua majengo ya karakana na mbao hazijaletwa ili kuendelea na upauaji wa majengo sita" amesema.
Mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) wilayani humo utagharimu shilingi Bil. 1.48 kwa awamu ya kwanza ambapo hadi sasa jumla ya shilingi Mil. 429.1 zimepokelewa na kwamba Mradi huo unatekekezwa Kwa kutumia mapato ya ndani chini ya Wizara ya fedha.
Mwisho.
Post a Comment