Na Derick Milton, Itilima.
Benki ya NMB kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya
ya Itilima Mkoani Simiyu, imekuwa benki ya kwanza nchini kuanza kutekeleza
mfumo mpya unaojulikana kama “Wezesha” wa utolewaji wa mikopo ya asilimia 10
kwa vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu kwenye Halmashauri.
Mfumo huo mpya ambao umeanzishwa na serikali unatekelezwa
katika Halmashauri 10 nchini kama majaribio, ambapo Halmashauri ya Wilaya ya
Itilima ikiwa moja wapo na imekuwa ya kwanza kuanza kutekeleza mfumo huo.
Kupitia mfumo huo Benki hiyo ya NMB pamoja na
Halmashauri hiyo wamefanikiwa kutoa mkopo wa Sh Milioni 117 kwa vikundi 15 vya
wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kutoka katika kata 8 za Halmashauri
hiyo.
Akizungumza katika Hafla ya utolewaji wa mikopo kwa
mfumo huo iliyotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa Halmashauri hiyo,
Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri Amina Mbwambo alisema kuwa mfumo unalenga
kuondoa changamoto zilizokuwepo kwenye mikopo hiyo.
Alisema kuwa mfumo huo unalenga kuboresha uwajibikaji,
ufuatiliaji pamoja na urejeshwaji mikopo kwa wakati, ambapo awali wanufaika
wengi walikimbia na mikopo hiyo hali ambayo serikali iliamua kuja na mfumo huo.
“ Kwenye Halmashauri 10 za mfano nchini Halmashauri
yetu ya Itilima tumewakuwa wa kwanza kuanza kutekeleza kwa kushirikiana na
benki ya NMB, ambapo vikundi vinaomba mkopo kupitia mfumo huo na kuhakikisha na
kamati tatu pamoja na beki,” alisema Mbwambo.
Afisa Maendeleo huyo alisema katika kuanza kutekeleza
mfumo huo, jumla ya vikundi 25 viliomba mkopo wenye thamani ya Sh Milioni 445
kupitia mfumo huo, ambapo baada ya uhakiki kupitia kamati mbalimbali pamoja na
benki ya NMB vilibaki vikundi 15 ambavyo vimepatiwa mkopo wa Sh Milioni 117.
“ Uhakiki huu ulikuwa unafanyiwa wazi, vikundi hivyo
vilihakikiwa na kamati ya mikopo ngazi ya kata, Halmashauri, Kamati ya uhakiki
ngazi ya Wilaya kisha Benki ya NMB, na leo vimepatikana vikundi 15 kati ya 25
ambavyo viliomba,” alisema Mbwambo.
Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Magharibi Restus
Assenga alisema kuwa awali benki hiyo ilipokea jumla ya vikundi 16 kutoka
Halmashauri ambapo walifanya uhakiki na kubakiza vikundi 15 ambavyo vilikidhi
vigezo.
Alisema kuwa jumla ya vikundi 6 vya wanawake vimepewa
Mkopo wa Sh Milioni 46, Vijana vikundi 6 ambavyo vimepata mkopo wa Sh Milioni
55 na wenye ulemavu vikundi vitatu ambavyo vimepata mkopo wa Sh Milioni 17.3.
“ Kwa kushirikiana na watalaamu wa Halmashauri Benki ya
NMB inaendelea kutoa elimu kwa wanufaika jinsi ya kusimamia fedha, elimu ya
biashara pamoja na elimu ya kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha, lengo waweze
kunufaika na mkopo huo,” alisema Assenga.
Mkuu wa Wilaya hiyo Anna Gidalya akizungumza wakati wa
hafla hiyo aliwataka wanufaika kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii ili
kuhakikisha wanaresha fedha hizo za mkopo ili ziweze kuwanufaisha wengine.
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya alisema atafuatilia kwa
ukaribu vindi vyote kuona shughuli ambazo wanazitekeleza kama kweli ni zile
ambazo waliombea mkopo huku akipiga marufu fedha hizo kuzibadilishie matumizi.
“ Nimuombe Mkaguzi wa ndani kuwa karibu na vikundi
hivi, kila mara vikaguliwe na kuangaliwa, lengo ni kupunguza migogoro na ugomvu
wakati wa kugawana faida, shughuli zao zikaguliwe na matumizi ya fedha pia,”
alisema Gidalya.
MWISHO.
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com
Post a Comment