NMB yaanza kutekeleza mfumo mpya utolewaji mikopo asilimia 10.

Meneja wa NMB Kanda ya Magharibi Restus Assenga ( kushoto aliyevaa suti) na Mkuu wa Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu Anna Gidalya (Kulia mwenye miwani) wakikabidhi mfano wa hundi kutoka benki ya NMB ya mkopo wa Sh Milioni 117 kwa vikundi vya wanawake, vijana na wenyewe ulemavu 15 kutoka katika Halmashauri hiyo, vikundi hivyo vimenufaika na mkopo wa asilimia 10 unaotokana na makusanyo ya mapato ya ndani. (Picha na Derick Milton)

 



Na Derick Milton, Itilima.


Benki ya NMB kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu, imekuwa benki ya kwanza nchini kuanza kutekeleza mfumo mpya unaojulikana kama “Wezesha” wa utolewaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu kwenye Halmashauri.


Mfumo huo mpya ambao umeanzishwa na serikali unatekelezwa katika Halmashauri 10 nchini kama majaribio, ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Itilima ikiwa moja wapo na imekuwa ya kwanza kuanza kutekeleza mfumo huo.


Kupitia mfumo huo Benki hiyo ya NMB pamoja na Halmashauri hiyo wamefanikiwa kutoa mkopo wa Sh Milioni 117 kwa vikundi 15 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kutoka katika kata 8 za Halmashauri hiyo.


Akizungumza katika Hafla ya utolewaji wa mikopo kwa mfumo huo iliyotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa Halmashauri hiyo, Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri Amina Mbwambo alisema kuwa mfumo unalenga kuondoa changamoto zilizokuwepo kwenye mikopo hiyo.


Alisema kuwa mfumo huo unalenga kuboresha uwajibikaji, ufuatiliaji pamoja na urejeshwaji mikopo kwa wakati, ambapo awali wanufaika wengi walikimbia na mikopo hiyo hali ambayo serikali iliamua kuja na mfumo huo.


“ Kwenye Halmashauri 10 za mfano nchini Halmashauri yetu ya Itilima tumewakuwa wa kwanza kuanza kutekeleza kwa kushirikiana na benki ya NMB, ambapo vikundi vinaomba mkopo kupitia mfumo huo na kuhakikisha na kamati tatu pamoja na beki,” alisema Mbwambo.


Afisa Maendeleo huyo alisema katika kuanza kutekeleza mfumo huo, jumla ya vikundi 25 viliomba mkopo wenye thamani ya Sh Milioni 445 kupitia mfumo huo, ambapo baada ya uhakiki kupitia kamati mbalimbali pamoja na benki ya NMB vilibaki vikundi 15 ambavyo vimepatiwa mkopo wa Sh Milioni 117.


“ Uhakiki huu ulikuwa unafanyiwa wazi, vikundi hivyo vilihakikiwa na kamati ya mikopo ngazi ya kata, Halmashauri, Kamati ya uhakiki ngazi ya Wilaya kisha Benki ya NMB, na leo vimepatikana vikundi 15 kati ya 25 ambavyo viliomba,” alisema Mbwambo.


Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Magharibi Restus Assenga alisema kuwa awali benki hiyo ilipokea jumla ya vikundi 16 kutoka Halmashauri ambapo walifanya uhakiki na kubakiza vikundi 15 ambavyo vilikidhi vigezo.


Alisema kuwa jumla ya vikundi 6 vya wanawake vimepewa Mkopo wa Sh Milioni 46, Vijana vikundi 6 ambavyo vimepata mkopo wa Sh Milioni 55 na wenye ulemavu vikundi vitatu ambavyo vimepata mkopo wa Sh Milioni 17.3.


“ Kwa kushirikiana na watalaamu wa Halmashauri Benki ya NMB inaendelea kutoa elimu kwa wanufaika jinsi ya kusimamia fedha, elimu ya biashara pamoja na elimu ya kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha, lengo waweze kunufaika na mkopo huo,” alisema Assenga.


Mkuu wa Wilaya hiyo Anna Gidalya akizungumza wakati wa hafla hiyo aliwataka wanufaika kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha wanaresha fedha hizo za mkopo ili ziweze kuwanufaisha wengine.


Aidha Mkuu huyo wa Wilaya alisema atafuatilia kwa ukaribu vindi vyote kuona shughuli ambazo wanazitekeleza kama kweli ni zile ambazo waliombea mkopo huku akipiga marufu fedha hizo kuzibadilishie matumizi.


“ Nimuombe Mkaguzi wa ndani kuwa karibu na vikundi hivi, kila mara vikaguliwe na kuangaliwa, lengo ni kupunguza migogoro na ugomvu wakati wa kugawana faida, shughuli zao zikaguliwe na matumizi ya fedha pia,” alisema Gidalya.


MWISHO.

 


Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم