Na COSTANTINE MATHIAS, Katavi-Tanganyika
WAKULIMA wa Pamba kutoka Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi wameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali kulinda na kutunza vitalu vya uzalishaji wa mbegu za Pamba, kwa lengo la kuhakikisha ubora wa mbegu unaendelea kudumishwa na kuongeza tija katika kilimo cha zao hilo.
Wakulima hao kwa kushirikiana na Maafisa Ugani wa Wilaya hiyo, wameeleza dhamira yao ya kulinda kitalu hicho kwa kuhakikisha hakuna uchafuzi wa mbegu unaofanyika, hali ambayo itasaidia kuendeleza sifa nzuri ya Wilaya ya Tanganyika kama mzalishaji wa mbegu bora za Pamba nchini.
Akizungumza kuhusu hali ya utunzaji wa kitalu cha mbegu, Mkaguzi wa Pamba wa Wilaya ya Tanganyika, Focus Bugelaha, alisema kuwa juhudi za pamoja kati ya Serikali na wakulima zimeboresha kwa kiasi kikubwa ubora wa Pamba inayozalishwa wilayani humo.
Alisema kuwa wamejipanga vyema kuhakikisha uchafuzi wa Pamba unadhibitiwa kwa ukamilifu ili kulinda ubora wa mbegu hizo.
“Tumejipanga kusimamia ubora kwa kuwa Tanganyika ni eneo maalum la kuzalisha mbegu za Pamba...Tunasimamia kwa kushirikiana na Maafisa Ugani pamoja na programu ya BBT (Building a Better Tomorrow), ili kuhakikisha Pamba ya Katavi inakuwa bora zaidi na inakidhi viwango vya kitaifa,” alisema Bugelaha.
Aidha, Bugelaha alieleza kuwa katika hatua za kudhibiti uchafuzi, vituo vitatu vya ununuzi wa Pamba tayari vimepigwa faini kwa mujibu wa sheria na kwamba hatua hiyo imeongeza uwajibikaji na kuleta mabadiliko chanya katika jamii ya wakulima.
“Mwaka 2024 baadhi ya wakulima walivuna kati ya kilo 300 hadi 500 kwa ekari, lakini kutokana na elimu waliyopata na mwitikio mzuri wa matumizi ya teknolojia, msimu wa 2025 wakulima wengi wanatarajiwa kuvuna kati ya kilo 800 hadi 1,500 kwa ekari,” aliongeza Bugelaha.
Kwa mujibu wa takwimu za Wilaya, mwaka 2024 jumla ya kilo milioni 3.1 za Pamba zilivunwa na kwamba Mwaka huu wa 2025, kutokana na maboresho yaliyofanyika, wanatarajia kuvuna zaidi ya kilo milioni 7.
Wakulima wa Kijiji cha Kapanga, Kata ya Katuma, Wilaya ya Tanganyika walieleza kuwa wao ni mashahidi wa mabadiliko makubwa yanayoletwa na elimu ya kilimo bora cha Pamba.
Mkulima, Joseph Makambu, alieleza kuwa wako tayari kufuata kikamilifu maelekezo ya Serikali ili kuhakikisha mbegu zinazozalishwa zinakuwa bora na kuleta manufaa kwa wakulima na Taifa kwa ujumla.
“Kwa kuwa Serikali imetutenga kwa ajili ya kuzalisha mbegu za Pamba, ni jukumu letu kuhakikisha tunafuata kila maelekezo ya kitaalamu ili kulinda ubora wa mbegu hizo,” alisema Makambu.
Naye mkulima Magolanga Gervas, alisisitiza umuhimu wa kuzingatia ubora wa Pamba kwa kuepuka kuchanganya na vitu visivyofaa kama mchanga au maji ambayo huongezwa kwa lengo la kuongeza uzito.
Kwa upande wa sekta ya viwanda, Meneja wa Kiwanda cha kuchambua Pamba cha NGS kilichopo Mpanda, Kashilila Mwita, alisema kuwa viwanda vinaendelea kuchakata Pamba kwa kuzingatia madaraja tofauti kulingana na ubora, hatua ambayo inasaidia kutunza thamani ya Pamba inayozalishwa.
“Tumeanza uchakataji wa Pamba na tumeona tofauti kubwa kwenye ubora kutokana na elimu waliyopewa wakulima kuhusu njia sahihi za kilimo na uvunaji. Pamba safi hutengeneza nyuzi bora zaidi,” alisema Mwita.
Mwita aliongeza kuwa wameendelea kuelimisha Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) kuzingatia ubora wanaponunua Pamba kutoka kwa wakulima kwa kuepuka kununua Pamba iliyochafuliwa.
“Tunaendelea kusisitiza kuwa Pamba ikichanganywa na uchafu inapoteza ubora wake, hivyo lazima kila mdau wa sekta hii awajibike,” aliongeza Mwita.
Juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wizara ya Kilimo, TCB na programu ya BBT, kwa kushirikiana na wakulima na wadau wa viwanda, zinaendelea kuzaa matunda katika kuhakikisha ubora wa Pamba unaongezeka.
Wilaya ya Tanganyika inaendelea kuonesha mfano bora wa usimamizi wa vitalu vya mbegu, jambo ambalo linatarajiwa kuongeza mapato ya wakulima na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa Taifa kupitia mauzo ya Pamba yenye ubora wa hali ya juu.
Mwisho.
Post a Comment