Na Samwel Mwanga, Maswa.
MCHAKATO wa kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ajili ya kumpata mgombea wa ubunge katika Jimbo la Maswa Mashariki umehitimika kwa ushindi wa kishindo kwa Dkt. George Lugomela, ambaye aliibuka kinara kwa kupata kura 4,759.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CCM wilaya ya Maswa, Efreim Kolimba ambaye ni Katibu CCM wilaya hiyo ametangaza matokeo hayo leo Agosti 5,2025.
Lugomela, ambaye ni mtaalamu wa rasilimali za maji na aliwahi kuhudumu kama Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji katika Wizara ya Maji, amempiku kwa tofauti ya kura 1,671 aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo na Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo, aliyepata kura 3,088.
Wagombea wengine waliokuwa wakichuana ni pamoja na Dkt. Adolf Saria aliyepata kura 373, George Mayunga aliyepata kura 369, huku mgombea mwingine na Nyangi Kimori, akipata kura 20.
Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi, Dkt. Lugomela amesema kuwa anawashukuru wanachama wa chama hicho kwa ushindi mkubwa alioupata.
“Ninawashukuru wanachama wa CCM kwa imani kubwa waliyonionesha. Ushindi huu si wangu binafsi bali ni wa wananchi wa Maswa Mashariki. Kama chama kitaniteua rasmi, naahidi kuwatumikia kwa bidii, uadilifu na kujituma kwa ajili ya maendeleo ya kweli.”amesema.
Katika baadhi ya vituo vya kupigia kura, hususan vijijini, wanachama wa CCM walieleza kuwa sababu kubwa ya mabadiliko ni kiu ya kuona sura mpya yenye dira ya maendeleo na ushirikiano mpana na jamii.
“Tunamhitaji kiongozi anayetoka na sisi mashinani, anayefahamu shida za wakulima, wafugaji na vijana. Dkt. Lugomela tunaamini ana uwezo huo,” amesema Mwalu John, mkazi wa Lalago.
Mchakato wa kura hizo uliosimamiwa na CCM Wilaya ya Maswa ulifanyika kwa utulivu, ingawa katika baadhi ya maeneo kuliripotiwa changamoto ndogo ndogo ambazo hata hivyo hazikuathiri matokeo kwa ujumla.
Matokeo haya sasa yanasubiri uamuzi wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, itakayopitisha jina la mgombea rasmi wa chama hicho kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Mwisho.


Post a Comment