Matumaini Mapya, ujenzi kituo Cha kupozea umeme Simiyu.

MKUU wa Mkoa wa Simiyu Dkt. Yahaya Nawanda (Kushoto) akizungumza na Wakandarasi wanaotekeleza mradi wa ujenzi wa kituo cha kupozea Umeme wa njia kuu yenye msongo wa KV 220.

Aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati, Medard Kalemani akiweka jiwe la Msingi ujenzi wa kituo cha kupozea umeme eneo la Imalilo Mkoani Simiyu Machi 03, 2021.


 

Na Derick Milton, Simiyu.

 

Hatimaye matumaini mapya yameanza kuonekana kwa wananchi wa Mkoa wa Simiyu, juu ya ujenzi wa kituo cha kupoza umeme (Sub station) baada ya wakandarasi wa mradi huo kuanza kutekeleza kazi za awali.

 

Mradi huo unatekelezwa na wakandarasi wawili, ambapo mmoja anatekeleza mradi wa ujenzi wa Njia kuu ya kusafirisha umeme ya msongo wa KV 220 Shinyanga hadi Simiyu na Mkandarasi wa pili anatekeleza ujenzi wa mradi wa kituo cha kupozea umeme.

 

Machi 03, 2021 aliyekuwa Waziri wa Nishati wakati huo Medard Kalemani, aliongoza hafla ya uwekaji jiwe la Msingi ujenzi wa kituo hicho eneo la Imalilo Mjini Bariadi na kutoa matumaini kwa wananchi wa Mkoa huo, kuondokana na adha ya kukatika mara kwa mara kwa umeme mara baada ya kukamila kwa mradi huo.

 

Kalemani alihaidi kituo hicho kujengwa ndani ya Mwaka mmoja, ambapo matumaini yalikuwa ujenzi huo ukamilike Machi 03, 2022, na ulitarajia kugharimu zaidi ya Sh. Bilioni 75.

 

Hata hivyo mradi huo haukuwahi kutekelezwa tangu kuwekwa kwa jiwe hilo msingi ikiwa imepita zaidi ya miaka mitatu huku matumaini ya wananchi wa Mkoa huo kuondokana na adha ya umeme kukatika katika mara kwa mara yakianza kupotea.

 

Matumaini hayo mapya yameanza kuonekana chini ya Rais Samia Suruhu Hassan baada ya Juzi Mkuu wa Mkoa huo, Dkt. Yahya Nawanda kufanya ziara katika Wilaya za Maswa na Bariadi ambako mradi huo unatekelezwa na kuzungumza na wakandarasi.

 

Ziara hiyo ya Mkuu wa Mkoa imefufua matumaini hayo na kwamba sasa mradi huo umeanza kutekelezwa, ambapo alitembelea kambi za wakandarasi hao na kuzungumza nao.

 

Akitoa taraifa ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo, Meneja mradi Mhandisi Adolf Kigombola alisema kuwa kazi za awali zimeanza kutekelezwa na mkandarasi baada ya TANESCO kwa kushirikiana na wadau wa mradi kufanya uhamasishaji kwa Wananchi ili kuruhusu uanzaji wa kazi za awali wakati Serikali ikichakata malipo ya Fidia.

 

Alisema kuwa TANESCO inafuatilia kwa karibu malipo ya fidia kwa waathirika wa mradi na kwamba Wananchi watarajie malipo ya fidia mapema Mwezi Novemba 2023.

 

Mkuu wa Mkoa aliwataka wakandarasi hao kuhakikisha wanatekeleza mradi huo, ndani ya muda uliopangwa, ili wanancha wa Mkoa wa Simiyu waweze kuondokana na adha ya kukatika katika kwa umeme mara kwa mara.

 

"Tunataka ndani ya miezi 18 kipindi cha Mkataba mradi uwe umekamilika na utekelezaji wa mradi usiwe na mashaka mashaka na wamenihakilishia hapa kuwa kazi hii itakamilika ndani ya muda uliopangwa" alisema Dkt. Nawanda

 

Mkandarasi M/S Kalpataru Projects International Limited (KPIL) kutoka Nchini India anatekeleza ujenzi wa Njia kuu ya kusafirisha umeme ya Msongo wa KV 220 na M/S Sian Electric Engineering Co.LTD akitekeleza ujenzi wa kituo cha kupozea umeme.

 

MWISHO.


Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post