MRADI WA MAJI BULYASHI KUHUDUMIA WANANCHI 2,725.

KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025, Ismail Ussi akikinga Maji mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika Mradi wa Maji Bulyashi wilayani Meatu ambao umetekelezwa kwa gharama ya Shilingi Mil. 662.


Na COSTANTINE MATHIAS, Meatu.


WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilayani Meatu Mkoani Simiyu wametekeleza Mradi wa Maji katika Kijiji cha Bulyashi kwa gharama ya shilingi Mil 662 ambao utanufaisha wananchi 2,725.


Mradi huo umetajwa kuwa mwarobaini wa tatizo la Maji katika kijiji hicho, kwani awali wananchi walikuwa wanatumia Maji yasiyo safi na salama wakichangia na Mifugo jambo ambalo liliwasababishia magonjwa ya tumbo, kuhara na kipindupindu.


Akizungumza mara baada ya kukagua na kuweka jiwe la Msingi ujenzi wa Mradi huo, Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Isamail Ussi amesema kipaumbele cha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuboresha miundombinu katika sekta ya Maji na kwamba RUWASA wana Mamlaka ya kusambaza Maji vijijini.


Kiongozi huyo wa mbio za Mwenge, amewataka wananchi kutunza miundombinu ya Maji ili kuondoa changamoto za ukosefu wa Maji ambazo zilizokuwa zinawakabili katika maeneo yao.


Katika hatua nyingine, Ussi amewataka wananchi kujitokeza katika Uchaguzi Mkuu ili waweze kupata viongozi Bora ambao watatekeleza miradi mbalimbali ya Maendeleo.


Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Simiyu Mhandisi Emmanuel Luswetula amewataka Wananchi kutunza miundombinu ya Maji ambayo inagharimu fedha nyingi kuwafikishia huduma ya Maji safi na salama.


Ameeleza kuwa, awali wananchi walikuwa wanachota Maji mtoni sababu hapa kuwa na Miundombinu ya Maji ambapo hadi sasa wanapata Maji kwa asilimia 85 na kwamba wamejipanga kuhakikisha wanafikisha huduma za Maji katika maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma ya Maji safi na salama.


Ameongeza kuwa katika wilaya ya Meatu, jumla ya miradi sita yenye thamani ya shilingi Bil. 6.2 inaendelea kutekelezwa ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya Maji kwa mujibu wa Ilani ya CCM.



Akiwasilisha taarifa ya Mradi huo, Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilaya ya Meatu, Mhandisi Davidi Kaijage amesema kuwa mradi wa Bulyashi umetekelezwa katika Kijiji Cha Bulyashi ili kuwaondolea wananchi adha ya kutembea mbali mrefu pamoja na kutumia Maji yasiyo safi na salama.


"Mradi huu unagharimu Shilingi Mil.662 na utahudumia wananchi 2,725 pamoja na taasisi tano ambazo zitanufaika na Mradi huo" amesema Meneja huyo.


Ameeleza kuwa, kabla ya Mradi huu, Kijiji hicho hakikuwa na huduma ya Maji na kwamba wananchi walikuwa wanatembea umbali mrefu kutafuta huduma ya Maji ambayo hayakuwa safi na salama na yaliwasababisha mlipuko magonjwa ikiwemo ugonjwa wa matumbo, kuhara na kipindupindu.


Holo Shema, mkazi wa Kijiji cha Bulyashi anasema awali walikuwa wanatumia Maji yasiyo safi na salama kutoka kwenye visima hali iliyowasababishia kuugua tumbo pamoja na watoto kuharisha.


"Huko nyuma Maji yalikuwa machafu sana, ukitumia unaumwa tumbo na watoto kuharisha...tunashukuru sana kupata haya Maji ambayo ni safi na salama, tunamshukuru Rais Samia na Wasaidizi wake kutusogezea huduma ya Maji ambayo imetufikia hadi majumbani" anasema Hollo.


Naye Neema Salehe, mkazi wa Bulyashi anasema kabla ya Mradi huo yeye na Wananchi wenzake walikuwa wanafuata Maji mtoni ambayo siyo safi na salama pia Maji hayo walichangia na mifugo (Ng'ombe) hivyo yalikuwa yananuka mkojo.


Anaishukuru serikali serikali kwa kutekeleza.mradi huo ambao umewasogezea huduma.ya Maji karibu na maeneo ya makazi yao.


Mwisho.


Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025, Ismail Ussi akimpongeza Mkuu wa Wilaya ya Meatu Faudhia Ngatumbura kwa Usimamizi mzuri wa miradi ya Maendeleo.












Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم