MWENGE WA UHURU WAZINDUA MIRADI YA AFYA NA ELIMU ITILIMA.

 

Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa mwaka 2025,Ismail Ussi (aliyeko kati) akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ntangaswa wilaya ya Meatu mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho.


Na Samwel Mwanga, Itilima


MWENGE  wa Uhuru 2025 umeendelea kuacha alama ya maendeleo katika Wilaya ya Itilima, Mkoani Simiyu, baada ya kuzindua miradi miwili mikubwa ya kijamii yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 300, ikiwemo Zahanati ya Ntangaswa na Shule ya Sekondari Shikizi Ng’wang’wita.


Zahanati ya Ntangaswa, iliyojengwa kwa nguvu za wananchi na kusaidiwa na serikali kwa Sh milioni 104 katika awamu ya kwanza, inatarajiwa kuhudumia wakazi 2,564 wa kijiji hicho na vitongoji jirani. Hapo awali, wananchi walilazimika kutembea takribani kilomita sita kufuata huduma za afya katika Kijiji cha jirani cha Mwalushu.


Kiongozi wa Kitaifa wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025, Ismail Ussi, akiweka jiwe la msingi katika zahanati hiyo Agosti 11,2025 amesema kuwa mradi huo ni ishara ya mshikamano wa dhati kati ya wananchi na serikali.


"Tunatarajia huduma za afya zitaboreshwa kwa kiwango kikubwa, na changamoto ya akina mama wajawazito kutembea umbali mrefu itabaki historia," amesema.


Hali hiyo inathibitishwa na mkazi wa kijiji hicho, Helen Jacobo, ambaye aliwahi kujifungua njiani akielekea kwenye zahanati ya mbali ya kijiji cha Mwalushu.


"Kwa kweli hii zahanati imenipunguzia hofu na mateso niliyoyapitia. Ni faraja kubwa kwa kina mama wote wa Ntangaswa kwani mimi niliwahi kujifungulia njiani wakati nikiwahishwa katika zahanati ya kijiji cha Mwalushu ,"amesema.


Awali akisoma taarifa ya mradi huo,Ester Msigala amesema kuwa kukamilika kwake kutaboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wa kijiji hicho na vijiji jirani.


“Kuwepo kwa zahanati hii kutapunguza vifo vya akinamama wajawazito na watoto walio chini ya miaka mitano kwani huduma za afya watazipata karibu na maeneo yao,”amesema.


Kwa upande wa elimu, Mwenge wa Uhuru pia umezindua Shule ya Sekondari Shikizi Ng’wang’wita, iliyojengwa ili kupunguza changamoto ya umbali kwa wanafunzi waliokuwa wakisoma katika Sekondari ya Nkoma, umbali wa zaidi ya kilomita 13.5 kwenda na kurudi kila siku.


Shule hiyo, yenye madarasa mawili ya kisasa, ofisi ya walimu imegharimu zaidi ya Sh milioni 53, fedha zilizotokana na michango ya wananchi sh milioni 13.4 na Halmashauri ya Wilaya Sh milioni 39.7 kupitia mapato ya ndani.


Mwanafunzi wa kidato cha kwanza, Geofrey Richard, amesema mradi huo umemwondolea usumbufu mkubwa wa kusafiri masafa marefu kila siku.


"Sasa nitapata muda zaidi wa kusoma badala ya kutumia masaa mengi njiani. Hii shule imenisaidia sana mimi na wenzangu," alisema.


Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Anna Gidarya, aliwataka wananchi kuhakikisha miradi hiyo inalindwa na kuendelezwa.


"Miradi hii si mali ya mtu binafsi bali ni urithi wa kizazi cha sasa na kijacho. Ni jukumu letu kuilinda na kuisimamia," amesema.


Miradi hiyo miwili ni sehemu ya utekelezaji wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025 katika Wilaya ya Itilima, ambapo miradi zaidi ya Sh bilioni 3.1 imezinduliwa na kuwekwa mawe ya msingi katika sekta mbalimbali ikiwemo maji, barabara na maendeleo ya jamii.


MWISHO. 











Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم