Na
Derick Milton, Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi amewaagiza
makatibu tawala wa mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga kuhakikisha kabla ya
mwezi Oktoba, 2025 maafisa ugani kwenye halmashauri zao wawe wamefika kwenye
kituo cha kuzambaza teknologia za kilimo (TARI NYAKABINDI).
Alisema kuwa maafisa ugani hao wafike kwenye kituo hicho
kilichopo Wilayani Bariadi Mkoani Simiyu kwa ajili ya kujifunza teknologia na
mbinu za kisasa za kilimo kwa ajili ya kuwasaidia wakulima wazalishe kwa tija.
Mkuu huyo wa Mkoa ametoa maagizo hayo juzi wakati akifunga
maonyesho ya Nanenane kanda ya ziwa Mashariki yaliyokuwa yanafanyika kwenye
viwanja vya Nyakabindi Wilayani Bariadi Mkoa wa Simiyu.
Alisema kuwa kituo hicho kimekuwa kikitoa mafunzo
mbalimbali hadi kwa wakulima na maafisa ugani, ya jinsi ya kuzalisha kwa tija
hivyo ni muhimu maafisa hao kupata elimu hiyo.
“ Nitumie nafasi hii kuwaagiza makatibu tawala wa mikoa
ya Simiyu, Mara na Shinyanga, kuhakikisha hadi mwezi Oktoba mwaka huu maafisa
ugani kwenye halmashauri zenu waje hapa TARI Nyakabindi wajifunze teknologia za
kisasa za kilimo,” alisema Kanali Mtambi…
“ Maafisa hao wakipata elimu hiyo wataweza kuitumia kwa
wakulima kwenye maeneo yao ya kazi, watawafundisha teknologia hizo za kisasa na
wakulima watabadilika na kuanza kwa tija, lakini pia watawasaidia kupata mbegu
bora,” aliongeza Kanali Mtambi.
Awali akiwa katika banda la Taasisi ya utafiti wa
kilimo chini (TARI) kwenye maonyesho hayo, Mkuu huyo wa Mkoa alipata maelezo
kutoka kwa msimamizi wa kituo hicho cha TARI Nyakabindi Isabera Mrema.
Msimamizi huyo wa Kituo alimweleza Mkuu huyo wa Mkoa
kuwa kituo hicho kimekuwa kikitoa mafunzo mbalimbali kwa maafisa ugani,
wakulima na wadau wengine wa kilimo juu ya teknologia za kisasa.
“ Tunaomba maafisa ugani kwenye hii kanda yetu waje
hapa tuwape mafunzo mbalimbali ya teknologia za kisasa, ili waweze kuwasaidia
wakulima kuzalisha kwa tija,” alisema Mrema.
MWISHO.
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com
إرسال تعليق