VIPANDO MAONESHO NANENANE NYAKABIDI KIVUTIO KWA WANANCHI.

 

Mkulima wa zao la pamba, Lupande Nhila (wa kwanza kushoto) akitoa maelezo ya vipando vya pamba kwa viongozi walioongozwa na Rc Simiyu, Anamringi Macha (wa pili kulia) kwenye viwanja vya nanenane Nyakabindi.


Na Samwel Mwanga, Bariadi.


MAMIA ya wananchi wameendelea kumiminika katika viwanja vya maonesho ya Nanenane kanda ya ziwa mashariki vilivyoko Nyakabindi, mkoani Simiyu, huku wakivutiwa na vipando vya mfano vya mazao mbalimbali yanayooneshwa katika mashamba darasa.


Baadhi ya wananchi wakizungumza leo Agosti 5,2025 katika viwanja hivyo wakati wa uzinduzi wa maonesho hayo wameeleza kuwa  vipando hivyo vimekuwa kivutio kikubwa kwa wakulima waliotoka mikoa ya Simiyu, Mara, na Shinyanga.


 Maria Mwikwabe mkulima kutoka katika wilaya ya Tarime mkoa wa Mara amesema kuwa amejifunza kwa vitendo kuhusu mbegu bora na matumizi sahihi ya viuatilifu.


"Nimevutiwa sana na mbegu za mahindi ya muda mfupi zilizopandwa hapa. Pia nimeelezwa namna ya kupambana na magonjwa kwa kutumia njia zisizo na sumu kali. Hii imenifungua macho sana.” amesema.


Masunga Mipawa ni mkulima kutoka katika wilaya ya Kishapu mkoa wa Shinyanga amesema kuwa amejifunza jinsi mbolea za asili na za viwandani, pamoja na mbinu za kisasa za kilimo cha umwagiliaji katika mazao hasa ya chakula.


Naye Lupande Nhila ambaye ni mkulima wa zao la pamba katika kijiji cha Senani wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu amesema kuwa mbegu zilizotumika katika mashamba darasa hayo yanaweza kuongeza uzalishaji wa zao hilo kwa ekari moja.


Mabula Gimu ni Kaimu Afisa Kilimo wilaya ya Maswa amesema kuwa wamekuwa wakitoa elimu juu ya mbegu zilizoboreshwa za zao la pamba.


Tumeandaa mashamba darasa yanayoonyesha tofauti ya mavuno kati ya mbegu za kawaida na zile zilizofanyiwa utafiti. Lengo ni kuwasaidia wakulima kufanya maamuzi sahihi kisayansi.”amesema.


Akizungumza wakati wa kukagua vipando hivy, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha, aliwataka wananchi kutumia fursa ya maonesho hayo kama darasa la kujifunza mbinu mpya za kilimo, ufugaji na uvuvi.


"Tunaamini kuwa kwa kujifunza hapa, mkulima akienda kutumia alichojifunza kwenye shamba lake, ataongeza tija na kipato. Maonesho haya si ya kutazama tu, ni ya kubadili maisha,” amesema.


Amesema kuwa serikali inaendelea kuwekeza katika tafiti za kilimo, miundombinu ya umwagiliaji, pamoja na kuhamasisha matumizi ya teknolojia ili kuongeza uzalishaji na usalama wa chakula.


Mbali na taasisi za serikali, sekta binafsi pia imeonesha ubunifu mkubwa, hasa katika kuonesha zana rahisi za kilimo kama mashine za kupandia, mashine za kuchakata pamba na mfumo wa kisasa wa umwagiliaji kwa matone.


Maonesho ya Nanenane Nyakabindi yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa wakulima, wafugaji, taasisi za utafiti na sekta binafsi kukutana na kubadilishana maarifa. 


Wananchi wengi wamepongeza maandalizi ya mwaka huu na kuahidi kuyatumia mafunzo hayo kwa ajili ya kubadilisha kilimo chao.


Mwisho.


Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Anamringi Macha (wa pili kushoto) akipata maelezo juu ya matumizi ya zana za kilimo katika viwanja vya Nanenane, Nyakabindi.


Viongozi wa serikali wa mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Mara wakitembelea vipando vya mazao mbalimbali katika viwanja vya Nanenane, Nyakabindi mkoa wa Simiyu.






Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post