25,000 hawajaripoti kidato cha kwanza Simiyu.

Wanafunzi.

Ofisa Elimu Mkoa wa Simiyu, Mwl. Majuto Njanga.


Na Bahati Sonda, Simiyu.


Jumla ya wanafunzi 25,328 kati ya 32,700 waliochaguliwa kujiunga na elimu ya Sekondari kidato cha kwanza shule za kutwa kwa muhula wa masomo mwaka 2023 katika Mkoa wa Simiyu bado hawajaripoti shuleni.


Ofisa Elimu Mkoa wa Simiyu Mwl. Majuto Njanga amesema kuwa hadi kufikia Januri 13, 2023 wanafunzi 7,372 sawa na asilimia  22.7 ndiyo walikuwa wameripoti shuleni toka shule zifunguliwe Januri 09, 2023.


Mwl. Njanga ametoa taarifa hiyo mapema jana kwenye kikao kazi cha mapitio ya tathimini ya Utekelezaji wa shughuli za uboreshaji na usimamizi wa elimu Mkoa wa Simiyu, kilichofanyika katika ukumbi wa Kusekwa Mjini Bariadi.


Amesema kuwa serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria ya elimu kwa mzazi yeyote atakayebainika kusita kumpeleka mtoto shule kupata haki hiyo muhimu bila sababu.


" Wazazi wa wanafunzi waliochaguliwa tunawasihi wahakikishe wanawapelekwa shuleni watoto wao kuripoti ili waweze kudahiliwa kwa muda unaotakiwa bila kujali changamoto yeyote inayomkabili" amesema Njanga


Amesema kuwa ofisi yake imetoa taarifa kwa vyombo vyote vinavyohusika, vikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa vijiji na kata, ili watoto wote waliocaguliwa kuhakikisha wanakwenda shule.


" Tumetoa maagizo kwa viongozi wote wa shule, watoto wasiweke vikwazo vyovyote, wapokelewe shuleni na kuanza masomo, hata kama mwanafunzi hana sare za shule, aanze na sare zake za shule ya msingi, wakati wazazi wakiendelea kumtafutia sare zinazotakiwa" amesema Ofisa Elimu.


Amesema kuwa serikali hapa nchini inataka watoto wote waliochaguliwa wanadahiliwa bila kujali changamoto yeyote ili kutoa fursa kwa mtoto kuanza masomo yake kwa wakati hivyo kumuwezesha kuwa na umahiri unaotakiwa.


Katika hatua nyingine Ofisa Elimu huyo amebainisha kuwa kiwango cha ufaulu wa wanafunzi katika mtihani wa kumaliza elimu ya Msingi kwa mwaka 2022 mkoa kimeshuka kwa asilimia 5.26 ikilinganishwa na mwaka 2021 ambapo ufaulu ulikuwa asilimia 85.52 .


Awali akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Lupakiso Kapange ameonya wanasiasa wanaoingilia masuala ya elimu na kusisitiza kuwa watoto wote waliochaguliwa na walifikia umri wa kwenda shule na waliochaguliwa wote waende.


Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Elimu ya Awali ya Msingi Mwalimu Susana Nussu akimwakilisha Naibu Katibu Mkuu Elimu Ofisi ya Rais TAMISEMI amewataka walimu kusimama kwenye nafasi zao kuyatekeleza na kuyatenda yote waliyoelekezwa katika kikao hicho kwani wao ndio waliopewa dhamana ya kuwapa elimu bora watoto.


 Naye Katibu wa Tume ya Utumishi wa walimu ( TSC) Mwalimu Paulina Nkwama amesema kuwa suala la uandikishaji wa wanafunzi wa awali na darasa la kwanza ufanyike kulingana na matokeo na kwamba udahili wa kidato cha kwanza uendane na ufaulu wao huku akisisitiza kuwekwa mkazo kwa wa ufundishaji wa somo la kiingereza kuanzia darasa la 3 kwani kufanya hivyo kutawarahisishia katika ujifunzaji pindi wanapojiunga na elimu ya sekondari.


    Mwisho.

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post