Kwa mara ya kwanza, Chungu cha Bawawa wapata Zahanati.



Na Anita Balingilaki, Bariadi.


Wakazi wa kijiji cha Chungu cha Bawawa kilichopo kata ya Nkololo wilayani Bariadi mkoani Simiyu wameeleeza kufurahishwa  na ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho ambapo wamesema itawapunguzia adha ya kwenda umbali mrefu wa takribani kilomita 15 kwa ajili ya kupata huduma za afya.


Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho wamesema  wagonjwa na akina mama wajawazito walikuwa wakitembea umbali mrefu kwa ajili ya kufuata huduma za afya hivyo  uwepo wa zahanati hiyo utakuwa na mkombozi wao huku wakiiomba serikali kuhakikisha uwepo wa dawa na watumishi wa kutosha pindi itakapokamilika.


“kwa ujenzi wa zahanati hii tunapunguza shida na umbali wa kumsogeza mgonjwa katika huduma hasa akinamama wajawazito ambao mara nyingine unawakuta  wanapata shida nyakati za usiku ambapo usafiri kwa shida kufika eneo la huduma lakini jengo hili litakapokuwa limekamilika na huduma zikianza mambo yatakuwa mazuri sana.” amesema Zacharia Susanya.


“serikali ituletee watumishi wa kutosha kwenye zahanati yetu hii na dawa za kutosha ili huduma itolewe vizuri  na wananchi wanufaike na uwepo wa zahanati hii kijijini hapa.” amesema Kasili Magagaa.


Kwa upande wake afisa mtendaji wa kijiji hicho Balumbilwe Mashimba ameishukuru serikali kwa kutoa shilingi milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati hiyo ambayo kwa sasa inaelekea kukamilika.


“sisi zahanati hii kwetu wana Chungu cha Bawawa ni mkombozi mkubwa kwasababu mama anaweza kujisikia akatembea tu kwa mguu kuja hapa kuliko ilivyokuwa hapo awali, kutoka Chungu cha Bawawa kwenda Nkololo ni kilomita 15 mama anayeumwa uchungu hawezi akafika kwa mguu ni mpaka usafiri, …usafiri wenyewe  ni shida.. tunamshukuru sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea zahanati hii .” amesema Mashimba.


Diwani wa kata ya Nkololo Emmanual Nyawela ameeleza kufurahishwa kwake na ujenzi wa zahanati hiyo ambayo inatarajiwa kuondoa adha ya upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi huku mkuu wa wilaya ya Bariadi Lupakisyo Kapange amesema kuwa madaktari na manesi wapo tayari kwa ajili ya kuhudumu katika zahanati hiyo mara tu itakapokamilika.


“tunamshukuru mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwasababu tayari madaktari na manesi kwa ajili ya zahanati hii wamekwisha gawiwa kwa ajili ya kuja kuanza kutoa huduma katika zahanati hii itakapokamilika.” amesema Kapange.

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post