Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange akitoa maelekezo kwa viongozi wa Wilaya ya Itilima na Mkoa wa Simiyu, mara baada ya ziara yake ya siku moja Wilayani humo leo. |
Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange akikagua baadhi ya majengo katika Hospitali ya Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu. |
Na Derick Milton, Itilima.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange
ameagiza viongozi wa Wilaya ya Itilima na Mkoa wa Simiyu, kuhakikisha hadi
kufikia Februari 01, 2023 kituo cha Afya Mwanunda kinaanza kufanya kazi na
wananchi wanapata huduma.
Kituo hicho ambacho kipo katika Wilaya hiyo, baadhi ya
majengo yamekamilika ujenzi wake asilimia 100, ambapo Naibu Waziri amesema
watalaamu Idara ya Afya Wilaya na Mkoa washirikiane na kuhakikisha hadi kufikia
muda huo kituo kinaanza kufanya kazi.
Dkt. Dugange ametoa maagizo hayo leo alipofanya ziara ya siku
moja Wilayani huyo na kutembelea ujenzi wa kituo hicho, huku akiridhishwa na
ujenzi wa majengo yaliyokamilika na kueleza kuwa yanaendana na thamani ya pesa.
Amesema kuwa hadi kufikia tarehe hizo, mganga mkuu wa Wilaya
na Mkoa, wahakikishe dawa zinakuwepo kwenye kituo hicho pamoja na watoa huduma
ili wananchi waanze kupata huduma haraka iwezekanavyo.
Amesema kuwa ameelezwa kuwa kuchelewa kutoa huduma kwa kituo
hicho inatokana na kutokamilika kwa taratibu za usajili, ambapo ameelekeza
watalaamu hao kufuatilia usajili Wizara ya Afya ndani ya wiki moja.
“ Ndani ya wiki mganga mkuu wa Wilaya na wa mkoa, mshirikiane
kituo kipate usajili, tumekubaliana hadi tarehe 01 Februari, 2023 wananchi
waanze kupata huduma hapa, hivyo hakikisheni dawa zinakuwpo, vifaa tiba na
watalaamu” amesema Dkt. Dugange.
Aidha Naibu Waziri huyo amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri
hiyo Elzabert Gumbo kuhakikisha huduma ya maji inakuwepo kituoni hapo, pamoja
na huduma ya umeme.
“ Tumeona hapa hakuna huduma ya umeme, pamoja na Maji, Mkuu
wa Wilaya amesema atafanyia kazi huduma ya umeme, Mkurugenzi hakikisha huduma
ya maji inakuwepo hapa kabla ya kituo hakijaanza kufanya kazi, lakini
kamilisheni baadhi ya majengo ambayo bado hajakamilika,” amesema Dkt. Dugange.
Awali akisoma taarifa ya ujenzi wa kituo hicho Kaimu Mganga
mkuu Wilaya hiyo Oswin Mlelwa amesema kuwa serikali ilitoa kiasi cha Sh.
Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho.
Amesema kuwa halmashauri ilipokea kiasi hicho na kuanza
ujenzi, ambapo jengo la wagonjwa wa nje, maabara, na kichomea taka yamekamilika
asilimia 100 huku ujenzi ukiendelea kwenye jengo ya wodi ya wazazi, jengo la
kufulia pamoja na jengo la upasuaji.
Baadhi ya wananchi waliozungumza mbele ya Naibu Waziri
wameishukuru serikali kwa kuwaletea kituo cha Afya, kwani awali walikuwa
wakiangaika kwenda Wilayani Bariadi kupata huduma.
“ Tulikuwa tunakwenda Wilaya ya Bariadi kupata huduma, akina
mama wajawazito wamepoteza maisha na watoto wao, kutokana na umbali lakini
miundombinu ya Barabara kutokuwa rafiki” amesema Ng’wandu Masatu.
MWISHO.
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com
Post a Comment