Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Mwanaume mmoja mkazi wa mtaa wa kalonga kata ya Ngokolo katika Manispaa ya Shinyanga anashikiliwa na Jeshi la Polisi akidaiwa kuhusika na tuhuma za mauaji ya Mke wake Joyce Masanja ambaye anasadikiwa ameuawa kwa kuchomwa kisu.
Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo Jumamosi Januari 14,2023 ambapo mwili wa mwanamke huyo umekutwa ukiwa umetelekezwa jirani na msikiti wa Binti haji uliopo Mtaa wa Kalonga kata ya Ngokolo.
Waandishi wa habari wamefika katika eneo la tukio na kuzungumza na wakazi wa mtaa wa kalonga jina maarufu Mshikamano ambao wameeleza kuwa tukio hilo limetokea majira ya saa sita usiku ambapo baadhi yao wamesikia sauti ya marehemu huyo akikimbizwa na watu wawili huku akipiga kelele.
Majirani wamesema baada ya kusikia kelele hizo kwa muda mfupi umeme ulikatika na kwamba hawakusikia tena kelele ndiyo asubuhi walimkuta Joyce Masanja amefariki Dunia pembezoni mwa barabara jirani na msikiti wa Binti haji.
Baadhi ya wananchi waliofika kwenye tukio hilo wameeleza kuwa wamekuta marehemu huyo amefariki Dunia huku akiwa amechomwa kisu sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwepo sehemu ya shingo, kwenye ubavu pamoja na sehemu ya mapaja yake.
Wameeleza kuwa wamesikitishwa na tukio hilo ambapo wameilalamikia serikali ya mtaa huo kuwa wanatoa mchango wa fedha kila mwezi kwa ajili ya ulinzi shirikishi na kwamba ulinzi huo haufanyiki ipasavyo huku wakiliomba jeshi la polisi kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha mauaji ya Mwanamke huyo Joyce Masanja
Post a Comment