Waondokana na adha ya kusaka maji kwenye madimbwi, mabwawa.


MKUU wa wilaya ya Bariadi Lupakisyo Kapange akitwishwa ndoo ya Maji kichwani na akina mama katika mtaa wa mbiti kama ishara ya kuwatua ndoo akinamama mara baada ya serikali ya awamu ya sita kuwasogezea huduma ya maji karibu na maeneo yao.


 

MKUU wa wilaya ya Bariadi Lupakisyo Kapange akitwishwa ndoo ya Maji kichwani na akina mama katika mtaa wa mbiti kama ishara ya kuwatua ndoo akinamama mara baada ya serikali ya awamu ya sita kuwasogezea huduma ya maji karibu na maeneo yao.



Wakina mama wakazi wa mbiti katika Halmashauri ya mji wa Bariadi wakichota maji kwenye kituo cha kuchotea maji. (Picha zote na COSTANTINE MATHIAS).


Na Costantine Mathias, Bariadi.

WANANCHI wa Vijiji vya Ngulyati, Mbiti, Dutwa na Sengerema wilayani Bariadi mkoa wa Simiyu wameipongeza serikali kwa kuwajengea miradi ya maji katika maeneo yao, jambo ambalo limewapunguzia adha ya kusaka maji katika mito, madimbwi, vijito na mabwawa.

 

Aidha wamesema kipindi cha nyuma walikuwa wanatumia maji yasiyo safi na salama jambo ambalo lilikuwa linawasababishia kuugua magonjwa ya tumbo, kuhara, kichocho na minyoo lakini kwa sasa wanakunywa maji safi na salama na hawapati madhara kiafya.

 

Wakizungumza na waandishi wa habari, waliotembelea miradi ya Maji inayotekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wamesema wanaipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kuwasogezea huduma ya maji kwa lengo la kuwatua ndoo wakinamama.

 

Suzana Sayi, mkazi wa Mbiti anasema mradi wa maji katika eneo lao umewanufaisha wanawake ambao huko nyuma walikuwa wakifuata maji bwawani kwa umbali mrefu wakiwa wamebeba watoto mgongoni, lakini kwa sasa wanapata maji karibu na makazi yao.

 

Naye Magreth Stephano mkazi wa Mbiti anasema kwa sasa wanapata maji karibu na makazi yao, na kwamba huko nyuma walikuwa wanahangaika kupata maji yaliwasababishia mlipuko wa magonjwa ya tumbo, kuhara na kichocho.

 

‘’Tunaishukuru serikali kutuletea mradi wa Maji haoa Dutwa, kwa sasa tunapata maji safi na salama…tunamshukuru Rais Samia Suluhu kwa kutukumbuka wanawake wenzake na kututa ndoo kichwani, huko nyuma tulihangaika sana kupata maji na kushindwa kufanya shughuli za kiuchumi’’ anasema Ester Charles mkazi wa Sengerema-Dutwa.

 

Awali akizungumza kuhusu ujenzi wa miradi huyo, Kaimu Meneja wa RUWASA wilaya ya Bariadi Mhandisi Marco Miko amesema mradi wa Mbiti una vituo 12 vya kuchotea maji, tenki lenye ujazo wa lita 50,000 na utanufaisha wakazi 5200 na umejengwa kwa gharama ya shilingi milioni 237.

 

Kuhusu mradi wa Ngulyati, Mhandisi Miko amesema utanufaisha vijiji vitatu vya Ngulyati, Nyamswa na Nyasosi, utakuwa na vituo vya kuchotea maji 18 na utahudumia watu 21,000 na kwamba mradu huo unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 1.3.

 

‘’mradi wa Dutwa umeshakamilika na wananchi wanapata maji, tumejenga vituo 18 vya kuchotea maji na watu 128 wameshaunganishiwa maji majumbani…mradi umejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 1.06, tunawaomba wananchi kuitunza miradi ya maji ili iweze kuwanufaisha’’ anasisitiza Mhandisi Miko.

 

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Lupakisyo Kapange ameishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu kwa kutekeleza ujenzi wa miradi ya maji kupitia RUWASA huku akiwataka wananchi kuitunza miradi hiyo ili iweze kuwanufaisha.

 

‘’Niwaombe wananchi tutunze miradi ya maji, Rais Samia ametoa fedha nyingi kwa ajili ya kuwatua ndoo akina mama, ametekeleza Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi…wajibu wetu ni kuilinda na kuitunza miradi hii ili ifikapo 2025 tumlipe kwa kwenye sanduku la kura’’ amesema Kapange.

 

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post