MKUU wa wilaya ya Maswa mkoani Simiyu,Aswege Kaminyoge amewataka viongozi wote wa serikali wilayani humo kuanzia ngazi ya kitongoji hadi wilaya kuwasimamia wakulima wa zao la pamba ili waweze kulima zao hilo kwa kufuata kanuni bora.
Amesema hayo katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya hiyo wakati akikabidhi pampu 658 za kupulizia sumu ya kuua wadudu wanaoshambulia zao la pamba likiwa shambani kwa Vyama vya Ushirika vya Msingi(Amcos)55 vilivyoko wilayani humo.
Amesema katika musimu huu wa kilimo wa mwaka 2022/2023 atachukua hatua kwa viongozi wote ambao watashindwa kutimiza wajibu wao wa kusimamia wakulima wa zao hilo ambao watalima bila kufuata kanuni bora za kilimo cha zao la pamba.
Amesema kuwa kushindwa kwa viongozi hao kusimamia kilimo bora cha zao hilo kwenye maeneo yao kumesababisha wakulima kulima kiholela zao la pamba ambalo lipo kwa mujibu wa sheria.
"Hili zao la pamba lipo kwa mujibu wa sheria za nchi na sio kienyeji sheria Na.2 ya mwaka 2001 na ile ya 2011 zilitungiwa kanuni 10, moja wapo ya kanuni inamtaka kila mkulima kung’oa na kuchoma maotea yote ya msimu uliopita ili kuua wadudu waharibifu kuhamia kwenye msimu mpya,kupanda kwa msitari pamoja na kupulizia dawa ya kuuwa wadudu," amesema.
Mkuu huyo wa wilaya ameagiza kuchukuliwa hatua za kisheria kwa wakulima wote waliokiuka taratibu za kilimo cha zao hilo na kuwasisitiza viongozi kutoona aibu kuisimamia sheria hiyo ya kilimo cha zao la pamba.
Amesema kuwa serikali ya awamu ya sita kwa kuona umuhimu wa zao hilo kwa wilaya hiyo imetoa sumu(viuadudu)bure kwa wakulima ili waweze kuzalisha kwa wingi kwani zao hilo ni muhimu kwa uchumi wa wilaya ya Maswa na mkoa wa Simiyu kwa ujumla.
Naye balozi wa zao la pamba hapa nchini,Agrey Mwanri amesema kuwa wakukima walio wengi wa zao hilo katika wilaya hiyo bado wanauelewa mdogo juu ya kulima kilimo chenye tija.
Amesema kutokana na hali hiyo imewalazimu waanzishe kuwepo mkulima mwezeshaji ambae atakuwa ni chombo kwa wakulima wengine kutoa elimu ya kutosha juu ya kilimo hicho wanachosisitiza.
"Hawa wakulima wawezeshaji watakuwa mfano kwa wakulima wengine za zao la pamba na kwa kufanya hivyo kutainua na kuongeza pato la mtu mmoja na taifa ikilinganishwa na musimu wa mwaka 2021/2022," amesema.
Mkuu wa Divisheni ya Kilimo,Mifugo,Uvuvi na Ushirika katika halmashauri ya wilaya ya Maswa,Robert Urasa amesema kuwa ununuzi wa pampu hizo umegharimu kiasi cha Sh Milioni 27.
Amesema kuwa fedha hizo zimetokana na ushuru wa zao hilo uliokuwa unalipwa na Makampuni ya ununuzi wa zao la pamba musimu uliopita kwa Sh 20/-kwa kila kilo moja.
ReplyForward |
إرسال تعليق