Na Samwel Mwanga,Maswa.
BAADHI ya wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari katika wilaya ya Maswa
katika mkoa wa Simiyu wameishauri serikali kuwaondoa Walimu wakuu wa Shule za
Msingi na Wakuu wa shule za sekondari watakaoshindwa kusimamia sheria ya
utoaji adhabu ya viboko katika shule zao.
Ushauri huo wameutoa wilayani humo wakati wakizungumza na
Waandishi wa habari juu changamoto zinazowakabili wanafunzi hao na
kusababisha udumavu wa ustawi wa watoto nchini Tanzania wanapokuwa
shuleni.
Walisema kuwa kwa sasa kumekuwa na wimbi la baadhi ya walimu wa shule hizo
wilayani humo kutoa adhabu ya viboko kwa wanafunzi bila kufuata utaratibu huku
viongozi hao wa shule wakiwepo na kushindwa kuchukua hatua kwani ndiyo
wasimamizi wakuu wa nidhamu za wanafunzi katika shule hizo.
Walisema kuwa wanafunzi wengi wamekuwa wakiumizwa kwa kupigwa na
viboko hivyo sehemu mbalimbali za miili yao kinyume cha sheria hali
ambayo inazua uadui kati ya mwalimu na mwanafunzi pamoja na mzazi
wake jambo ambalo halijengi mahusiano mema kwa pande hizo mbili.
“Binafsi adhabu ya viboko naiunga mkono kwani inasaidia
kurejesha nidhamu ya mwanafunzi lakini itumike kwa mujibu wa sheria
iliyoiweka na siyo kumchapa mwanafunzi sehemu mbalimbali za mwili na
kumsababishia maumivu makali na wengine hupelekwa hospitali na kulazwa na
utakuta kosa lenyewe labda kachelewa kufika shuleni kwa muda uliopangwa,”
‘Ni vizuri kabla ya kutoa adhabu hiyo Mwalimu ajaribu
kumhoji mwanafunzi sababu ya kufanya kosa hilo unaweza kugundua jambo
na ukamsaidia, unaweza kukuta tatizo liko kwa mzazi wala si kwa mwanafunzi
hivyo kumwadhibu ni sawa na kumwonea ni vizuri Wakuu wa Shule na Walimu
wakuu wakasimamia utoaji wa adhabu ya viboko katika shule
zao,”alisema Maria Joseph.
Walisema kuwa adhabu hiyo imekuwa ikilaumiwa na wananchi wengi
nchini kwa kuwa walimu katika kuadhibu sasa hawachapi viboko bali wengine sasa
wanapiga wanafunzi kwa ngumi na mateke.
“Kinachofanyika shuleni walimu wanakiuka taratibu na sheria zilizoainishwa
na Serikali ambapo mbali ya kuwapiga viboko visivyo na
idadi na mbaya zaidi wanapiga katika maeneo mbalimbali ya mwili
ya wanafunzi wa wanaodaiwa kutenda makosa mbalimbali lakini pia walimu
wa kiume wanawapiga wanafunzi wa kike ambapo sheria haisemi hivyo.
" Walimu waliopewa dhamana ya kusimamia shule hizo
wanahesabika kama wameshindwa kazi ya uongozi ya kusimamia shule” alisema
Masanja Mayunga.
Walisema kuwa sheria ya adhabu ya viboko mashuleni inaeleza wazi
kuwa mwanafunzi ataadhibiwa kuchapwa viboko pale itakapobainika kuwa kosa
alilofanya ni ovu na adhabu yake ni viboko au kufukuzwa shule na
si vinginevyo lakini utekelezaji wake umekuwa holela na matokeo
yake haimfanyi mwanafunzi kujutia kosa lake isipokuwa kuwa sugu na kujenga
mahusiano mabovu na mwalimu aliyemwadhibu.
Waliendelea kueleza kuwa sheria ya Mtoto ya mwaka 2009,
chini ya kifungu cha 13 (1) inakataza mtu kumsababishia mtoto mateso au
aina nyingine ya ukatili au kumpa adhabu zisizo za kibinadamu au
kumdhalilisha mtoto na kifungu kidogo cha (2) kinaeleza kwamba endapo
adhabu ni mbaya au ni kubwa kwa kiwango cha mtoto kulingana na
umri, hali ya kimwili, kiakili wake haitakuwa stahili kwa mtoto.
“Sheria ya adhabu ya viboko kwa wanafunzi mashuleni inatamka wazi
kuwa n viboko vinne tu vinavyoruhusiwa kwa wanafunzi wavulana kuchapwa
kwenye makalio na wasichana mikononi na mwalimu akitoa adhabu hiyo
anaagizwa aandike kitabuni kuonesha tarehe na idadi ya viboko na
aliyeadhibiwa lazima asaini kitabuni humo lakini haya yote
hayafanyiki,”alisema Japhet John.
Mmoja wa Maafisa Elimu katika Ofisi ya Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi
wilayani humo ambaye hakupenda jina lake liwe wazi Kwa kuwa si msemaji wa
Divisheni hiyo akizungumzia suala la adhabu hiyo alisema kuwa adhabu
ya viboko iliwekwa ili kutunza nidhamu kwa wanafunzi shuleni na
wanaadhibiwa kwa wanafunzi waliofanya makosa makubwa shuleni kwa kufuata
taratibu za utoaji wake.
Alisema kuwa sheria hii inamtaka Mwalimu Mkuu wa shule husika kutoa adhabu
ya viboko au kukasimisha mamlaka yake kwa umakini mkubwa kwa
mwalimu yeyote kutoa adhabu hiyo na mwalimu anayechaguliwa kutoa adhabu atakuwa
na mamlaka ya kutoa adhabu pale tu atakapopata idhini
ya mwalimu mkuu katika tukio husika.
Aliongeza kueleza kuwa kanuni ya 5 inataka kila adhabu ya
viboko inapotolewa kwa mwanafunzi kumbukumbu ya kutolewa kwa
adhabu hiyo sharti iwekwe kwenye kitabu, ikitaja jina la mwanafunzi,
kosa alilolifanya, idadi ya viboko na jina la mwalimu
aliyetoa adhabu na kumbukumbu hizo lazima zisainiwe na Mkuu wa shule.
"Adhabu ya vinoko bado ina umuhimu na inatumika katika shule za
msingi na sekondari hapa nchini na hii adhabu inapaswa kutolewa
kwa mwanafunzi ambaye amefanya makosa makubwa shuleni pia ina utaratibu
wake wa kuitoa hivyo nitumie fursa hii kuwaomba walimu wakuu
na wakuu shule kusimamia utaratibu wa utoaji adhabu ya vinoko
kuliko utoaji holela unaofanywa na baadhi ya walimu,”alisema.
Sheria ya Elimu Sura ya 353 marejeo ya mwaka 2002` Kifungu
cha 61(1)(v) kinampa mamlaka Waziri wa Elimu kutunga kanuni za
masuala mbalimbali zitakayokidhi utekelezaji wa masuala
ya sheria hiyo.
Kupitia mamlaka hiyo, moja ya kanuni zilizotungwa ni The
Education (Corporal Punishment) Regulation G.N.294 ya
Mwaka 2002, zinazotoa mwongozo wa kutoa adhabu ya
viboko ikielezea wakati wa kutoa adhabu pamoja na kiwango cha adhabu hiyo
kwa mwanafunzi.
MWISHO
Post a Comment