Na Derick Milton.
Benki ya NMB imevunja rekodi ya kupata faida kubwa kwa mwaka 2022 kiasi cha Sh. Bilioni 429 baada ya kodi, ikiwa ni ongezeko la asilimia 47 kulinganisha na mwaka 2021.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo Bi. Ruth Zaipuna akiwasilisha taarifa ya fedha ya mwaka 2022, amesema kuwa mwaka 2022 umekuwa mwaka ambao NMB imeweka historia kubwa nchini, ambapo ameeleza hali hiyo imetokana na ushirikiano mzuri kutoka kwa wateja wake na benki hiyo.
Amesema kuwa kwa mara ya kwanza katika muda wa miaka 25 ya historia ya NMB mapato ya jumla yalivuka Tilioni moja, baada ya kufikia Sh. Tilioni 1.2, ongezeko likiwa asilimia 23.
" Tumefanikiwa kupata faida baada ya kodi ya Sh. Bilioni 429 kwa mwaka 2022, Hii ni ongezeko la asimilia 47 kulinganisha na faida ya Bilioni 290 tuliyopata mwaka 2021. Hii ni mara ya kwanza taasisi ya fedha nchini kupata faida kubwa kiasi hiki," amesema Zaipuna.
Amesema kuwa sambamba na juhudi za kuongeza ukopeshaji, jumla ya mali za benki nazo pia zilivuka kiasi cha Sh. Tilioni 10 na kufikia Tilioni 10.25, ukuaji ambao amesema wa kasi wa mizania wa asilimia 18 kwa mwaka mzima.
Amebainisha kuwa mafanikio hayo yanatokana na uwekezaji wa hali ya juu ambao benki hiyo imekuwa ikifanya katika teknologia, nidhamu ya kutekeleza mpango mkakati, kuwa na wafanyakazi wenye weledi pamoja na mazingira wezeshi yaliyowekwa na serikali.
" Kutokana na mafanikio haya ambao benki imepata, kwa mwaka 2023 tumetenga kiasi cha Sh. Bilioni 6.2 kwa ajili ya kurudisha kwa jamii, ambapo kama Benki tutasaidia kwenye nyanja za Elimu ya fedha, Afya, Mazingira, Elimu, na ajenda endelevu kwa ujumla" amesema.
Post a Comment