Utatuzi wa migogoro unadumisha amani katika jamii.

 


Wadau wa Sheria katika wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu wakiwa kwenye maandamano siku ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria nchini.

Na Samwel Mwanga,Maswa.

 

UTATUZI wa migogoro kwa njia ya usuluhishi umeelezwa kuwa unadumisha amani,upendo na utulivu katika jamii

 

Hayo yameelezwa leo na Hakimu Mkazi  Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu,Enos Misana wakati akitoa neno la shukrani kwa Mkuu wa wilaya ya Maswa aliyewakilishwa na Afisa Tarafa ya Sengerema ,Saguda Sayayi kwenye Uzinduzi wa Wiki ya Sheria  wilayani humo.

 

Uzinduzi huo ulifanyika katika viwanja vya Mnadani mjini Maswa na kuhudhuria na Wananchi mbalimbali wakiwemo wanafunzi na walimu wa shule za sekondari zilizoko  mjini humo.

 

Hakimu Misana amesema kutokana na umuhimu huo wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi ambalo ni takwa la kikatiba ambalo utekelezaji wake ni vizuri iendane na kazi ya shughuli za ukuaji wa uchumi nchini.

 

"Masuala ya utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi hili linatajwa kwenye ibara ya 107(A)(2)(b)ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa msingi huo ni takwa la kikatiba hivyo ni vizuri wananchi wakalitambua,"amesema.

 

Amesema katika kipindi hiki cha wiki ya sheria hapa nchini maafisa wa mahakama hiyo watatoa elimu na hamasa kwa Umma juu ya umuhimu wa usuluhishi wa migogoro kwa kuwaongoza wananchi juu ya jambo hilo.

 

Hakimu Misana akielezea moja ya faida ya utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi ni pamoja na kufanya pande zote mbili zilizotofautiana kuwa wamoja Kwa sababu hakuna mshindi tofauti na kesi mahakamani ni lazima mmoja ashindwe.

 

"Kwenye kesi ni lazima mmoja ashinde na mwingine ashindwe hivyo aliyeshindwa atajenga chuki pamoja na uhasama kwa aliyeshinda lakini kwenye usuluhishi hakuna mtu atakayeshindwa na watamaliza tofauti zao kwa amani,"amesema.

 

Awali mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ya Maswa ambaye alikuwa mgeni rasmi,Sayayi amesema ni vizuri wananchi wajitokeze katika kipindi hiki Ili waweza kupata elimu kutoka kwa watumishi wa mahakama juu ya usuluhishi wa migogoro katika maeneo yao.

 

Amesema kusuluhisha migogoro kwa njia hiyo kutasaidia kupunguza kesi kwenye mahakama sambamba na muda ambao ungetumika kusikiliza kesi hizo.

 

Kaulimbiu ya Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria nchini ya mwaka huu ni"UMUHIMU WA UTATUZI WA MIGOGORO KWA NJIA YA USULUHISHI KATIKA KUKUZA UCHUMI ENDELEVU:WAJIBU WA MAHAKAMA NA WADAU".

 

MWISHO 

 

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post