Wananchi kata ya Shigala waondokana na kero ya daraja la miti.

 

Baadhi ya Wananchi wa kata ya Shigala wakipita kwenye daraja la Miti ambalo ni hatari kwa usalama wa Maisha yao.
 
 
Mbele; Daraja la Miti ambalo wananchi walikuwa wanatumia kama kivuko nyakati za Masika na nyuma ni daraja jipya lililojengwa na Wakala wa Barabara za Mjiji na Vijiji (TARURA) wilaya ya Busega kwa ajili ya kurahisisha mawasiliano, usafiri na usafirishaji.

 

Na COSTANTINE MATHIAS, Busega.

 

WANANCHI wa Vijiji vya Shigala na Ihayabuyaga, Kata ya Shigala wilayani Busega Mkoani Simiyu wameipongeza Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA) baada ya kuwajengea daraja lililounganisha mawasiliano na kufungua usafiri na usafirishaji.

 

Awali wananchi hao walikuwa wakitumia daraja la miti lililokuwa limejengwa kienyeji ili kuwawezesha kuvuka mto nyakati za masika hali ambayo ilikuwa inahatarisha usalama wa maisha yao.

 

Wakizungumza na Waandishi wa habari, wananchi hao wameipongeza serikali kwa kuwajengea daraja hilo ambalo limekuwa mkombozi na limegharimu kiasi cha shilingi mil. 183.

 

Dotto Makinga, Mwenyekiti wa kijiji cha Ihayabugaya, alisema huko nyuma mto huo ulitengenisha mawasiliano baina ya vijiji viwili hali iliyowalazimu kutengeneza kivuko cha miti ili kurahisisha mawasiliano na shughuli za kiuchumi za wananchi.

 

‘’wananchi walikuwa wanshindwa kuvuka katika mto huu kwenda kwenye shughuli za kilimo, ilitulazimu kuzunguka umbali mrefu…wanafunzi walishindwa kwenda shule nyakati za masika, tunaishukuru serikali kutujengea daraja hili na kurahisisha huduma za usafiri na mawasiliano’’ anasema Makinga.

 

Adam Buluma, mkazi wa Shigala aliipongeza serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia kwa kutoa fungu la kutekeleza adhma na ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

 

Alisema jamii na wananchi walishindwa kufanya shughuli za kimaendeleo kutokana na kizuizi cha mto huo, lakini walitengeneza daraja la muda la miti ambalo halikuwa salama ili wananchi waweze kupata huduma za kielimu na afya.

 

‘’Baada ya kupata fungu kutoka serikali kuu, TARURA wametengeza garaja imara ambalo linapitika muda wote na wananchi wanasafiri muda wote, wakati wa mikutano na kampeni viongozi walishindwa kuwafikia wananchi kutokana na changamoto ya daraja hilo’’ alisema Buluma.

 

Ester Yohana alisema kabla ya daraja hilo kujengwa walikuwa wanapata shida ya kusafiri kwenda zahanati hali iliyokuwa inawalazimu kutambaa wanapovuka kwenye daraja la miti.

 

Meneja wa Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA) wilaya ya Busega Mhandisi Mwita Mhochi alisema Barabara ya Busega-Mwamjulila yenye urefu wa kilometa 7.5 inaunganisha kata mbili za Shigala na Igalukilo.

 

Alisema barabara hiyo iliharibika na kuwafanya wananchi kushindwa kupata huduma hali iliyowalazimu wananchi kutengeneza daraja la miti kwa kushirikiana na diwani.

 

‘’Mwaka 2021/22 tulitenga bajeti ya mil. 183 ili kujenga daraja hili…tunaishukuru serikali ya Rais Samia kwa kutenga bateji hiyo ambapo kwa sasa ujenzi umekamilika na wananchi wanatumia daraja hilo’’ alisema Mhochi.

 

Alisema licha ya daraja hilo kukamilika, ujenzi wa barabara hiyo bado unaendelea ambapo wakala huo umetenga shilingi milioni 130 kwa ajili ya kuiwekea molamu kwa mwaka wa fedha 2022/23.

 

Aliongeza kuwa fedha za tozo zimetumika kujenga daraja hilo ambalo limekuwa mkombozi kwa wananchi na linafungua huduma za mawasiliano, usafiri na usafirihi.

 

Mhandisi Mhochi aliwataka wananchi kutunza daraja hilo ambalo limejengwa na serikali kwa gharama kubwa likilenga kuwahudumia kwa muda mrefu.

 

MWISHO.

 

 
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post