Maofisa kutoka Bodi ya Nyama nchini wakifanya ukaguzi wa Bucha za Nyama eneo la soko kuu la Bariadi Mkoani Simiyu jana. |
Maofisa kutoka Bodi ya Nyama nchini wakifanya ukaguzi wa Bucha za Nyama eneo la soko kuu la Bariadi Mkoani Simiyu jana. |
Na Derick Milton, Bariadi.
Wamiliki wa Bucha za Nyama katika Wilaya ya
Bariadi Mkoani Simiyu, wamepewa muda wa miezi miwili, kuhakikisha wanakidhi
vigezo vyote vya kutoa huduma hiyo, ikiwemo kuzingatia suala la usafi.
Hatua hiyo imekuja baada ya kubainika uwepo wa
Bucha nyingi katika Mji wa Bariadi ambako ni makao makuu ya Mkoa wa Simiyu,
kutokuwa katika hali nzuri ya utolewaji wa huduma hiyo.
Maofisa kutoka Bodi ya Nyama wakifanya ukaguzi jana kwenye bucha zote zinazouza nyama katika Mji wa Bariadi, walibaini makosa mengi huku suala la usafi likiwa halizingatiwi hata kidogo.
Msomi Antony ambaye ni Daktari kutoka Bodi ya
Nyama, alisema kuwa wamekuta Bucha nyingi hazitumii nondo nyeupe, hazina vigae,
wauzaji havai gambuti, havai makoti meupe wala kofia.
Aidha makosa mengine ni wauzaji kutokuwa na vyeti
vya Afya zao kama ambavyo inatakiwa, lakini bucha nyingi zikitumia nondo zenye
rangi jambo ambalo alisema ni hatari kwa Afya za walaji kwani inaweza kusababsha
ugonjwa wa kansa.
“ Tumekuta Bucha nyingi wametundika nyama nje ya
madirisha, suala ambalo ni marufuku nyama kuwekwa nje, lakini nyingi hazina
vioo, wanatumia magogo kukata nyama, hawana visu vinavyotakiwa, hawana mashine,
hali ambayo tumeona ni hatari kwa walaji” amesema Antony.
Maofisa hao wamesema kuwa wamebaini wauzaji na
wamiliki wa Bucha katika Mkoa wa Simiyu, wengi hawana elimu juu ya vigezo
vinavyotakiwa kwenye kutoa huduma hiyo, ambapo wametumia nafasi hiyo
kuwaelimisha.
“ Tumetumia muda huo pia kuwaelimisha na kuwataka
hadi kufikia tarehe 31/03/2023 wawe wamebadilisha vitu vyote ndani ya
bucha zao, leo hatukuja kufunga, lakini baada ya muda huo tutakuja na
opereisheni kali ya kufunga na kuwaondoa,” aliongeza Antony.
Naye Ofisa Mifugo kutoka Bodi hiyo Nemesiusi
Mkalaza amesema kuwa baadhi ya vigezo wamiliki wanakiuka kwa maksudi kwani ni
vitu vya kawaida hata kwenye familia zao huku akitolea mfano suala la usafi.
Amesema kushindwa kuzingatia suala la usafi kwenye
uuzaji wa nyama, ni hatari sana kwa walaji kwani wanyama wana magonjwa mengi
ambayo yanaweza kumshambulia binadamu ikiwa nyama haipikwa vizuri.
Mwisho.
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com
Post a Comment