CCM Waridhishwa na Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo Maswa.

Mkurugenzi wa Shirika la Reli nchini (TRC) Masanja Kadogosa (mwenye shati jeupe) akitoa maelezo ya Ujenzi wa Reli ya kisasa katika mji wa Malampaka wilayani Maswa Kwa wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Simiyu.

 

Kaimu Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu, Emanuel Silanga (wa kwanza kushoto) akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) mkoa wa Simiyu, Mhandisi John Mkumbo wa kwanza kulia, baada ya Kamati ya Siasa mkoa wa Simiyu kutembelea Ujenzi wa barabara ya lami ya mchepuko mjini Maswa.
 
 

Ujenzi tenki la kuhifadhi Maji lenye ukubwa wa Lita Mil. 2 linalojengwa na Mamalaka ya Maji na Usafi wa Mazingira (MAUWASA) katika Kijiji Cha Hinduki wilayani Maswa.

 

 

Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu wakikagua Ujenzi wa Upanuzi wa zahanati ya kijiji Nguliguli katika wilaya ya Maswa

 

 

Na Samwel Mwanga, Maswa.

 

KAMATI ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoa wa Simiyu imesema imeridhishwa na matumizi ya fedha na kasi ya utekelezaji wa miradi ya Maendeleo katika sekta mbalimbali wilaya ya Maswa.

 

Hayo yameelezwa na Kaimu Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu, Emanuel Silanga kwa nyakati tofauti akiwa na wajumbe wa kamati hiyo kwenye ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

 

Miradi iliyotembelewa ni pamoja na Ukarabati wa barabara ya Senani-Zebeya-Lalago, Ujenzi wa bwawa la Maji katika Kijiji cha Zebeya na Ujenzi wa tenki la kuhifadhi maji katika kijiji cha Hinduki.

 

Miradi mingine ni pamoja na ujenzi wa barabara ya mchepuko kwa kiwango lami mjini Maswa, Upanuzi wa zahanati katika kijiji cha Nguliguli na ujenzi wa reli ya kisasa katika kituo cha Malampaka.

 

Amesema kuwa ukarabati wa barabara ya Senani-Zebeya-Lalago yenye urefu wa kilomita 26.5 kwa thamani ya Sh milioni 340 hadi sasa kwa muonekano uko vizuri na unategemea kukamilika April 26, mwaka huu.

 

Akizungumzia ujenzi wa bwawa la Zebeya ameipongeza Wizara ya Maji kupitia Bonde la Ziwa Victoria kwa kukamilisha ujenzi huo na Kwa sasa bwawa hilo limejaa maji na kushauri ni vizuri sasa likabidhiwe rasmi kwa wananchi wa kijiji hicho Ili waweze kuyatumia maji hayo.

 

"Tuwapongeze Wizara ya Maji kupitia Bonde la Ziwa Victoria kwa kukamilisha ujenzi wa bwawa la Zebeya na sasa limejaa maji hivyo basi ufanyike utaratibu hili bwawa likabidhiwe Kwa Wananchi Ili waanze kunufaika na maji hayo kwa matumizi ya binadamu na mifugo," amesema Gungu na kuongeza.

 

"Tulisikia kulikuwa na mgogoro wa baadhi ya watu juu ya bwawa hili sisi CCM mkoa wa Simiyu tunasema bwawa hili ni zuri na wananchi walitumie kwa manufaa yao tunachotaka wananchi wapate maji si hayo malumbano yasiyo na tija wakati kazi imemalizika vizuri,’’.

 

Aidha amewataka wasimamizi wote wa miradi hiyo ambayo Bado haijakamilika kuhakikisha inamalizika kulingana na muda uliopangwa Ili iweze kuwanufaisha Wananchi.

 

Gungu ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC), wamempongeza Rais, Dkt Samia Kwa kutoa fedha nyingi Kwa ajili kutekeleza miradi hiyo hasa ukiwemo mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa.

 

"Hii miradi yote ni fedha kutoka serikallini ambayo iko chini ya Rais wetu, Dkt Samia Suluhu hivyo ni lazima tumpongeze ambaye pia ndiyo Mwenyekiti wetu wa CCM taifa Kwa kuruhusu hizo fedha kufika huku Simiyu na kutekeleza miradi ya maendeleo," amesema.

 

Naye Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Dkt Yahaya Nawanda amewasihi wananchi kuitunza miradi hiyo pindi itakapokamilika huku akitoa onyo kali kwa watu wote wenye tabia ya wizi wa vifaa vya Ujenzi hasa katika Ujenzi wa reli ya kisasa.

 

"Tumetangaza vita na wale watu ambao wanatabia ya kuiba vifaa vya Ujenzi kwenye miradi yetu mikubwa ya maendeleo kama Mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa Malampaka tumekomesha wizi wa mafuta na bado tunaendelea kupambana na wezi wote wa vifaa vya ujenzi kwenye reli yetu," amesema.

 

"Huu mradi wa reli ya kisasa ni wetu sisi Watanzania siyo wa Wachina Wala Wakorea hivyo tusaidiane kutoa taarifa za watu wote wenye nia ovu ya kuturudisha nyuma kutokana na wizi wa vifaa vya ujenzi kwenye Mradi huu wa reli,".

 

MWISHO.

 

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post